• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
Oliech adai angali mchezaji wa Gor Mahia

Oliech adai angali mchezaji wa Gor Mahia

Na CECIL ODONGO na MWANGI MUIRURI

MSHAMBULIZI wa zamani wa Harambee Stars Dennis Oliech ameshikilia kwamba yeye bado ni mchezaji halali wa Gor Mahia, hata baada ya uongozi wa klabu hiyo kukatiza kandarasi yake Jumanne jioni.

Oliech amesema kwamba hatambui barua aliyotumiwa na uongozi wa vigogo hao wa soka nchini, akisema hajakuwa akifika mazoezini kutokana na jeraha la mkono ambalo limekuwa likimtatiza tangu msimu jana.

“Hizi habari zote mnazosikia ni uongo na ukweli ulio dhahiri ni kwamba sijawahi kupona jeraha la mkononi. Hata bendeji ilitolewa majuma mawili yaliyopita, ningeweza kucheza kivipi ilhali mkono haujapona?” akauliza Oliech kwenye mahojiano ya kina na Taifa Leo.

Nyota huyo wa zamani ambaye alijiunga na K’Ogalo Januari mwaka huu alisisitiza kwamba habanduki kutoka mibabe hao wa soka nchini liwalo na liwe, akisema meneja wa timu Jolawi Obondo ndiye wa kulaumiwa kutokana na kusambaratika kwa mawasiliano kati yake na Gor Mahia.

“Watu wanasema kwamba sikuweza kufikiwa. Kwa nini hawakunitumia ujumbe kama kulikuwa na suala la dharura. Meneja wa timu anafahamu kwamba daktari wa timu alinishauri nisirejee mazoezini hadi nipone. Ni vibaya kwamba wanatamatisha kandarasi yangu ilhali mimi bado nina jeraha,” akaongeza Oliech.

Aidha alipuuza habari zilizodai kwamba alikuwa analenga kuwania kiti cha ubunge cha Kibra kwenye uchaguzi mdogo wa Novemba 7 na kushikilia hajawahi kutangaza kwamba anagombea wadhifa wowote wa kisiasa.

“Nimeshangazwa kuwa klabu imeniandikia kwamba nilikuwa na azma ya kuwania wadhifa wa kisiasa. Mimi si mpigakura Kibra wala sijui mtu aliyeweka picha yangu kwenye ukurasa wa facebook kuwa nagombea kiti hicho. Natoka eneobunge jirani la Dagoretti Kusini na sina haja na kuingia kwenye siasa isipokuwa katika Shirikisho la soka Nchini (FKF) siku zijazo,” akasema.

Akiwa na magoli 34 Oliech yuko kidedea katika utingaji mabao kwa taifa la Kenya.

Dennis Oguta Oliech 35 huthaminiwa na wengi nchini katika ulimwengu wa soka kama shujaa.

Oliech alipata ufanisi mfululizo katika maisha mwanzoni, lakini kwa sasa hali imeonekana kumyumbia si haba.

Kuna wanamshauri akome kufukuzana na maisha ugani kama kifaa, bali ajitose katika masomo ya ukufunzi na huenda ‘ajifufue’ kupitia mwanya huo.

Yanayodaiwa kuwa ni makosa ni Oliech kuwahi kujionyesha kama aliyetaka kugombea wadhifa wa ubunge katika eneo la Kibra katika uchaguzi mdogo uliozuka baada ya Ken Okoth kuaga dunia mapema mwezi huu na ambapo umeratibiwa kuandaliwa Novemba 7, 2019.

Oliech aliwahi kutajwa kuchapisha picha za kampeni akionekana akivalia shatitao lililo na nembo ya Klabu ya K’Ogalo.

Klabu ya Gor Mahia kimemtema nje katika tangazo la Jumanne usiku kwa msingi kuwa “nidhamu yake imesambaratika kupita kiasi cha kukubalika.”

Klabu hicho kimesema kuwa “ameshuka viwango ugani na huwa na mazoea ya kukosekana kwa maandalizi kumeishia uamuzi kuwa kanadarasi yake ya miaka miwili itamatishwe mapema hata kabla ya kuihudumia hata nusu yake.”

Alirejeshwa ugani na Gor Januari mwaka huu baada ya misururu ya kandarasi katika vilabu ugenini, akaanza kujipata kwa shida za ubora na hatimaye akarejea nchini ambapo alidaiwa kuwa mpenda anasa kiasi cha kuishiwa na hela.

Pia, Gor imegusia uamuzi wa Oliech wa ‘kuwania siasa’ kama sababu nyingine ya kumtema nje kwa msingi kuwa huenda aangazie klabu hiyo kama iliyo na msimamo wa kisiasa na chama.

Alianza usogora wake katika Klabu cha Mathare United kisha akajiunga na kile cha AJ Auxerre na aliporejea ugani akivalia jazi ya K’Ogalo, alitunukiwa mkataba wa kupokezwa Sh350,000 kwa mwezi.

Gor ilimtoa kutoka masaibu ya kandarasi kuyumba katika Klabu ya Dubai Cultural Sports Club katika ligi ya Kiarabu.

Kabla ya kutemwa nje, kulikuwa kumezuka mzozo mkuu kati yake na Gor Mahia, akiteta kuwa alikuwa amecheleweshewa malipo kwa kiwango cha Sh1.6 milioni.

Waratibu wa Oliech waliteta kuwa Gor ilikuwa ikimharibia jina sogora huyo ilihali “wanaelewa kuwa hawajakuwa wakimlipa pesa zake kwa mujibu wa kandarasi yake ya hadi 2021.

Kulikuwa na uvumi kuwa Oliech alikuwa amejiunga na Gor ili kujipa nafasi ya kuwakilisha Kenya katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika (Afcon) 2019 katika taifa la Misri, lakini hakufanikiwa.

Alizaliwa Februari 2, 1985, na aliwajibikia kiungo shambulizi na katika kilele chake, akasajiliwa na timu kadhaa za Ulaya, moja maarufu ikiwa ni Auxerre ya Ufaransa.

Alianza kucheza kabumbu katika timu ya Dagoretti Santos, akaingia Mathare United na akaibuka kama mtingaji magoli bora na hatimaye akapaa hadi kwa timu ya taifa akijipa umaarufu wa mbio kama umeme akiwa na mpira miguuni na hatimaye mashuti ya maangamizi ambayo nadra yalikuwa yakose kulenga nyavu zikatikisike.

Pia, amehudumia Klabu ya Nantes nchini Ufaransa.

  • Tags

You can share this post!

IKO SHIDA! ‘Kikosi cha Spurs hakijafikia kiwango cha...

Magavana kusimamisha huduma za kaunti zote 47

adminleo