• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Olivier Giroud abeba AC Milan dhidi ya Torino katika Ligi Kuu ya Italia

Olivier Giroud abeba AC Milan dhidi ya Torino katika Ligi Kuu ya Italia

Na MASHIRIKA

AC Milan walitamatisha msururu wa matokeo duni ya kutoshinda mechi saba mfululizo katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya fowadi Olivier Giroud kuwafungia bao la pekee na la ushindi dhidi ya Torino.

Giroud alipachika wavuni bao hilo katika dakika ya 62 baada ya kumegewa krosi na Theo Hernandez aliyepoteza fursa nyingi za wazi za kufungia Milan bao la pili kutokana na krosi za Rafael Leao.

Torino walianza mechi kwa matao ya juu na nusura wafunge bao kupitia kwa Antonio Sanabria aliyemwajibisha vilivyo kipa Ciprian Tatarusanu.

Milan watachuana na Tottenham Hotspur katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) nchini Italia mnamo Februari 14, 2023 kabla ya kushuka dimbani kwa ajili ya marudiano mnamo Machi 8, 2023.

Milan ambao ni mabingwa watetezi wa Serie A walimpanga mvamizi Zlatan Ibrahimovic, 41, katika kikosi chao cha akiba kwa mara ya kwanza msimu huu. Ibrahimovic alifanyiwa upasuaji wa goti mwishoni mwa msimu wa 2021-22.

Hata hivyo, hakuwajibishwa na kocha Stefano Pioli aliyeshuhudia kikosi chake kikipaa jedwalini kutoka nafasi ya sita hadi ya tatu japo wangali na alama 15 zaidi nyuma ya Napoli wanaoselelea kileleni mwa jedwali.

Milan hawakuwa wameshinda pambano lolote tangu Januari 4, 2023 walipotandika Salernitana 2-1 na walikuwa wamepoteza mechi nne mfululizo kabla ya kushuka dimbani dimbani dhidi ya Torino ugani San Siro.

Msururu wa matokeo yao bila ushindi ni pamoja na kichapo cha 1-0 dhidi ya Torino katika mchuano wa hatua ya 16-bora kwenye Coppa Italia mbele ya mashabiki wao wa nyumbani. Isitoshe, walipepetwa na Inter Milan 3-0 katika Italian Super Cup kabla ya Lazio na Sassuolo kuwadhalilisha kwa vichapo vya 4-0 na 5-2 mtawalia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Thiago Silva sasa kuchezea Chelsea hadi Julai 2024

Tundo, Carol Radull wapata kazi Safari Rally, Talanta Hela...

T L