• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Oparanya aachiliwa baada ya kuhojiwa kwa saa 2

Oparanya aachiliwa baada ya kuhojiwa kwa saa 2

NA SHABAN MAKOKHA

ALIYEKUWA Gavana wa Kakamega na naibu kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya ameachiliwa baada ya kuhojiwa kwa saa mbili katika kituo cha polisi cha Kakamega mnamo Alhamisi.

Bw Oparanya alikamatwa Alhamisi, Julai 13, 2023, na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) karibu na soko la Khayega kando ya barabara ya Kakamega-Kisumu.

Alipelekwa katika kituo cha polisi cha Kakamega chini ya ulinzi mkali ambako alihojiwa na maafisa wa DCI, huku malango ya kituo hicho yakiwa yamefungwa.

Wanahabari hawakuruhusiwa kuingia humo wakati Bw Oparanya alikuwa akihojiwa.

Akiongea baada ya kuachiliwa huru, Gavana huyo wa zamani aliwasuta maafisa kwa kuwa watundu akisema walimdhulumu na kumtisha.

“Nilipokaribia kituo cha kibiashara cha Khayega, magari matatu yenye nambari za usajili wa kibinafsi yalizuia gari langu na watu wakatoka wakinielekezea bunduki. Ni kama kwamba walikuwa wakimkamata gaidi. Walimvuta kando dereva wangu na kuchukua udhibiti wa gari langu. Hiki ni kitendo kibaya mno,” akasema Bw Oparanya.

Alisema wadai, wakati wa mahojiano, kwamba alitumia gari la serikali alipoongoza maandamano ya kupinga serikali katika kaunti za Bungoma na Busia.

“Walitaka niandikisha taarifa lakini nikakataa kutokana na jinsi walivyonikamata kwa njia ya kunidunisha. Badala yake wakili wangu Kennedy Echesa aliandikisha taarifa kwa niaba yangu,” akaongeza.

Bw Echesa alilaumu polisi kwa kumkamata gavana huyo wa zamani kama mfuasi wa Al-Shabaab na makundi mengine ya kigaidi.

“Tulimuuliza Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (eneo la Magharibi) atupe sababu za kukamatwa kwa Bw Oparanya. Lakini hakutoa sababu zozote isipokuwa kuongoza maandamano katika kaunti za Bungoma na Busia,” akasema Bw Echesa.

“Wamemwachilia huru bila masharti yoyote japo wamezuilia gari hilo na kumwagiza arejee kesho Ijumaa. Lakini tunawapa makataa ya saa 24 wamrejeshee Bw Oparanya gari hilo kwa sababu sio mali ya serikali. Ni mali aliyopewa chini ya Sheria ya Pensheni ya Kaunti ya Kakamega,” akasema.

Akiwahutubia wafuasi wake nje ya kituo hicho cha polisi, Bw Oparanya aliahidi kuongoza maandamano makubwa mjini Kakamega Jumatano wiki ijayo.

Aliwataka wakazi kujitokeza kwa wingi kupinga hatua ya serikali kupandisha ushuru, hatua ambayo imechangia kupanda kwa gharama ya maisha.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto adai Raila Odinga anataka Handisheki kupitia...

Lenolkulal yuko na kesi ya kujibu katika ufisadi wa Sh84.6...

T L