• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
Origi abeba Liverpool dhidi ya Wolves ligini

Origi abeba Liverpool dhidi ya Wolves ligini

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Divock Origi alitokea benchi na kufungia Liverpool bao la pekee na la ushindi dhidi ya Wolves mwishoni mwa kipindi cha pili katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi ugani Molineux.

Zikisalia sekunde za kuhesabu kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchuano kupulizwa, Origi alivurumisha langoni kombora kutokana na krosi ya Mohamed Salah na kuacha hoi kipa Jose Sa wa Wolves.

Bao la Origi liliwasisimua maelfu ya mashabiki wa Liverpool uwanjani huku kocha Jurgen Klopp akijitoma katikati ya uwanja kumkumbatia mwanasoka huyo raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Kenya.

Baada ya mechi, Klopp alishikilia kwamba Origi ni “nguli” wa soka ambaye “watu wataandika vitabu kumhusu” huku akisisitiza kuwa nyota huyo kwa sasa ni kipenzi kikubwa cha mashabiki uwanjani Anfield.

Ushindi wa Liverpool uliwapaisha hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL ambalo sasa linaongozwa na mabingwa watetezi Manchester City waliokung’uta Watford 3-1 baada ya Chelsea kupigwa 3-2 na West Ham United.

Kichapo kutoka kwa Liverpool kilikuwa cha uchungu mkubwa kwa Wolves waliobana kabisa safu yao ya ulinzi kwa zaidi ya dakika 94 japo wakafungwa chini ya sekunde 60 za mwisho wa mchezo.

Liverpool waliingia ugani kwa ajili ya mechi hiyo wakijivunia rekodi nzuri ya kufunga wastani wa mabao mawili katika kila mojawapo ya mechi zao 18 za awali na wakiwa wamepachika wavuni magoli 14 kutokana na mechi nne zilizopita.

Chini ya mkufunzi Bruno Lage, Wolves kwa sasa wanakamata nafasi ya nane jedwalini kwa alama 21 sawa na Manchester United. Kikosi hicho ambacho kitakachomenyana na Chelsea na Man-City kabla ya Krismasi, sasa hakijafunga bao katika mechi nane kati ya 15 zilizopita ligini msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real Madrid wacharaza Sociedad na kufungua pengo la alama...

EPL: Man-City watuma onyo kali kwa washindani wakuu ligini...

T L