• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
PAA kuhudhuria mkutano wa Raila Kasarani

PAA kuhudhuria mkutano wa Raila Kasarani

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Pan African Alliance (PAA), kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi, kimethibitisha kuwa wawakilishi wake leo watahudhuria mkutano wa Azimio la Umoja katika uwanja wa Kasarani, Nairobi.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na afisi yake kuu, chama hicho kilisema kuwa kinaunga mkono kauli mbiu ya umoja wa kitaifa kinachovumishwa na vuguvugu hilo linaloongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“PAA inaamini kuwa manifesto inayokumbatia ndoto za wanachama wake kote nchini, itaendelezwa na kufanikishwa katika mazingira ya umoja wa kitaifa, ambao ajenda kuu ya Azimio la Umoja,” ikasema taarifa hiyo.“Kwa sababu hii, PAA inasimama na vyama vingine vya kisiasa vyenye maono sawa na yake, viongozi na Wakenya kwa ujumla katika kuendeleza umoja wa taifa letu,” taarifa hiyo ikaongeza.

Hata hivyo, chama hicho ambacho kina mizizi yake katika eneo la Pwani ya Kenya, hakikubainisha ikiwa Gavana Kingi ni miongoni mwa watakaohudhuria mkutano wa leo, Kasarani.Mapema mwaka huu Gavana Kingi ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya ODM, alitofautiana na Bw Odinga kisiasa baada ya kuanzisha kampeni ya kuundwa kwa chama asilia cha Pwani.

Apokonywa wadhifa wake wa mwenyekiti wa ODM, Kilifi, ambao sasa unashikiliwa na Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire.Wakati huo huo, vinara wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA), Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka wamekwepo mkutano huo wa Kasarani.

Bw Mudavadi ambaye ni kiongozi wa ANC alisema amebanwa na shughuli zake za kibinafsi ilhali Bw Musyoka yuko Sudan Kusini kwa ziara rasmi.

You can share this post!

TAHARIRI: Dereva, abiria washirikiane kuzuia ajali msimu huu

Mtaa kwenye mpaka hata polisi waogopa!

T L