• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
NJENJE: Pakistan yaibuka mtumizi bora wa chai ya Kenya, yaishinda Uingereza

NJENJE: Pakistan yaibuka mtumizi bora wa chai ya Kenya, yaishinda Uingereza

Na WANDERI KAMAU

PAKISTAN ilinunua majanichai ya jumla ya Sh39.8 bilioni kufikia Oktoba 2021, hilo likiifanya kuwa nchi inayonunua zao hilo kwa wingi kutoka Kenya.

Takwimu kutoka Idara Kuu ya Kusimamia Majanichai nchini zinaonyesha kuwa taifa hilo lilinunua asilimia 37.1 ya majanichai yote ambayo Kenya iliuza ng’ambo.

Kiwango hicho ni ongezeko la Sh5.2 bilioni ikizingatiwa kwamba mnamo 2020, ilinunua majanichai ya Sh34.8 bilioni.

Takwimu pia zinaonyesha kuwa kiwango cha majanichai ambayo taifa hilo lilinunua kutoka Kenya kiliongezeka kutoka kilo 151.7 milioni hadi kilo 173.7 milioni.

Kijumla, Kenya iliuza kilo 467 milioni za majanichai kwa nchi mbalimbali mwaka 2021.

“Tuliuza kilo 467 milioni za majanichai kati ya Januari na Oktoba 2021 kwa nchi mbalimbali kutoka nje. Kiwango hicho ni ongezeko la kilo 39 milioni ikizingatiwa kuwa mnamo 2020, Kenya iliuza jumla ya kilo 428 milioni za majanichai katika muda kama huo,” ikasema idara hiyo.

Nchi kumi ambazo huwa zinanunua zao hilo kwa wingi kutoka kwa Kenya ziliongeza kiwango cha majanichai walizonunua isipokuwa Uingereza.

Katika muda huo, bei ya wastani ya kilo moja ya majanichai hayo ilikuwa Sh229 katika Soko la Majanichai la Mombasa.

Vile vile, Kenya ilipiga hatua kwani zao hilo liliuzwa katika maeneo 49 duniani, ikilinganishwa na maeneo 48 mnamo 2020.

Asilimia 89 ya majanichai hayo yaliuzwa katika nchi kumi ambazo huwa watumizi wakubwa wa zao hilo.

Mataifa hayo ni Pakistan, Uingereza, Sudan, Misri, Urusi, Iran, Nigeria, Uturuki, China kati ya mengine.

Ijapokuwa mataifa hayo ndiyo yamekuwa yakichangia pakubwa katika mapato ya Kenya kuhusu majanichai, serikali inasema imeanza kutafuta masoko mapya ili kuongeza pato la jumla la nchi.

Baadhi ya nchi ambazo zimeanza kununua zao hilo ni Ireland, Finland, Amerika na Ukraine.

Serikali imekuwa ikijaribu kuboresha mauzo ya zao nchini ijapokuwa kiwango cha matumizi yake miongoni mwa Wakenya bado kilo chini.

Takwimu zinaonyesha kuwa mnamo 2020, Wakenya walinunua kilo 33.7 milioni za majanichai.

Hata hivyo, kiwango hicho kilishuka na kufikia kilo 31 milioni mwaka 2021.

  • Tags

You can share this post!

Mtambo wa kuangua mayai wawaletea tuzo

Serikali kutumia Sh7 bilioni kuhamisha makaburi na...

T L