• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
Pambano kali kushuhudiwa Kiambu Ruto akikabili Uhuru

Pambano kali kushuhudiwa Kiambu Ruto akikabili Uhuru

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto sasa atakabana koo moja kwa moja na Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kiambaa, Kaunti ya Kiambu.

Hilo liliibuka jana baada ya chama cha People’s Empowerment Party (PEP) kutangaza kumwondoa mwaniaji wake, Raymond Kuria kwenye kinyang’anyiro hicho.

Badala yake, kilisema kitamuunga mkono John Njuguna, anayewania nafasi hiyo kwa chama cha UDA, kinachohusishwa na Dkt Ruto.

Vyama vya PEP na UDA viko katika mrengo wa ‘Hustler Nation’, unaomuunga mkono Dkt Ruto kuwania urais mwaka ujao.

Jana, Chama cha Jubilee (JP) nacho kilimtangaza Bw Kariri Njama kuwa mwaniaji wake katika eneobunge hilo, huku Bw Joseph Githinji akipeperusha bendera yake katika wadi ya Muguga, iliyo katika kaunti iyo.

Uchaguzi wa Kiambaa unaonekana kuwa jukwaa jingine la makabiliano ya kisiasa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto baada ya eneobunge la Juja (Kiambu) na wadi ya Rurii, Kaunti ya Nyandarua wiki iliyopita.

Kwenye uchaguzi wa Juja, Bw George Koimburi wa PEP aliibuka mshindi dhidi ya Bi Susan Njeri wa Jubilee. Katika wadi ya Rurii, Francis Muraya wa UDA alimshinda Bw Peter Thinji wa Jubilee.

Desemba mwaka uliopita, Jubilee pia ilipoteza kiti cha wadi ya Gaturi, Kaunti ya Muranga, baada ya Bi Esther Mwihaki wa PEP kuibuka mshindi dhidi ya Bi Rosemary Wakuthie wa Jubilee.

Wadadisi wanasema matokeo ya chaguzi hizo tatu yamempa Dkt Ruto ujasiri wa kumenyana na bosi wake.

“Matokeo haya ni muhimu sana wakati huu, ikizingatiwa siasa za urithi wa Rais Kenyatta zinaendelea kupamba moto. Ni muhimu vyama kudhihirisha vina ushawishi wa kutosha, hasa katika ngome zake,” asema Prof Macharia Munene.

Kulingana naye, kupenya kwa Dkt Ruto katika ngome ya Rais Kenyattta kunalenga kumdhihirishia rais kuwa hata yeye ana ushawishi licha ya juhudi ambazo zimekuwa zikiendelezwa kumkabili kisiasa na wandani wake.

“Ujumbe mkuu anaolenga kudhihirisha Dkt Ruto ni kuwa yeye ni mwanasiasa huru anayeweza kujisimamia bila baraka za Rais Kenyatta,” asema Prof Munene.

Wadadisi wanasema lazima Rais Kenyatta ahakikishe amefanya kila awezalo kuona Jubilee imehifadhi kiti cha Kiambaa, la sivyo hilo litakuwa pigo kubwa kwake.

“Kiambaa ni kama nyumbani kwa Rais. Litakuwa pigo kubwa ikiwa atashindwa. Ni hali itakayochora taswira ya mfalme aliyekataliwa kwake nyumbani,” asema mdadisi wa siasa Javas Bigambo.

You can share this post!

Maelfu watoroka makwao baada ya volkano kulipuka

Yaibuka raia wa Amerika aliteswa kisha kuuawa