• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Patrick Vieira akubali kuwa kocha wa Crystal Palace

Patrick Vieira akubali kuwa kocha wa Crystal Palace

Na MASHIRIKA

KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira amekubali kuwa mrithi wa kocha Roy Hodgson kambini mwa Crystal Palace na atatambulishwa rasmi kwa mashabiki wa kikosi hicho wakati wowote.

Palace walisalia bila mkufunzi baada ya Hodgson kuondoka uwanjani Selhurst Park mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Wengine waliokuwa wakiwania mikoba ya ukocha kambini mwa Palace ni Steve Cooper wa Swansea City na aliyekuwa mkufunzi wa Borussia Dortmund, Lucien Favre, 63.

Vieira alianza kuhusishwa na mikoba ya Palace mwanzoni mwa Aprili 2021 mkataba wa Hodgson, 73, ulipokuwa unaelekea kutamatika.

Akiwa sogora wa Arsenal, Vieira alinyanyua mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) chini ya kipindi cha miaka tisa. Kikosi chake cha mwisho kusimamia ni Nice inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Alipigwa kalamu mnamo Disemba 2020.

Vieira, 45, alistaafu kwenye ulingo wa soka akichezea Manchester City waliompa majukumu mepesi katika benchi ya kiufundi uwanjani Etihad kabla ya kupokezwa mikoba ya New York City FC inayoshiriki Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.

Aliongoza Nice kukamilisha kampeni za Ligue 1 kwenye nafasi ya saba jedwalini katika msimu wake wa kwanza kabla ya kutimuliwa baada ya miezi 18.

Baada ya kuagana na Arsenal, Vieira ambaye alisaidia Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mnamo 1998, aliwaongoza Inter Milan kutia kapuni mataji matatu ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kabla ya kuwanyanyulia Manchester City ubingwa wa Kombe la FA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Bustani ya Mama Ngina kufunguliwa Alhamisi

AKILIMALI: Biashara ya vyungu vya udongo inampa mwanga