• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
PCEA yapiga marufuku siasa makanisani

PCEA yapiga marufuku siasa makanisani

KANISA la Presbyterian Church of East Africa (PCEA) limepiga marufuku wanasiasa kupiga siasa kanisani muda mfupi baada ya Naibu Rais William Ruto kutumia kanisa hilo mtaani Umoja, Nairobi, kujipigia debe.

Kulingana na viongozi wa PCEA, marufuku hiyo haina uhusiano na Naibu Rais Ruto aliyeshiriki ibada katika kanisa lake la Umoja alipomshambulia kinara wa ODM Raila Odinga kwa kuwa ‘mnafiki’ kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi.

Dkt Ruto aliyekuwa ameandamana na wanasiasa mbalimbali wa Tangatanga, akiwemo mbunge wa zamani wa Starehe Margaret Wanjiru, pia alipuuzilia mbali wito wa kutaka Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022 uahirishwe.

“Hawa ndugu zetu ni watu wa ajabu sana kwa sababu wakiwa kwa serikali walikuwa wanaibia vijana. Sasa wako serikalini wanaibia wagonjwa wa Covid,’ akasema Dkt Ruto huku akimrejelea Bw Odinga.Marufuku hiyo ilitolewa na mkuu wa Kanisa la PCEA, Thegu Mutahi aliyekuwa akizungumza mjini Molo, Kaunti ya Nakuru.

Hatua hiyo ilifuatia kikao cha viongozi wa Kanisa la PCEA kilichofanyika mjini Molo ambapo waliafikiana kupiga marufuku wanasiasa kuzungumza siasa kanisani.

Viongozi hao walisema kuwa wanasiasa wataruhusiwa kuzungumza maneno machache iwapo watatumia fursa hiyo kuhimiza waumini kuhusu masuala ya kiroho kwa kutumia Biblia.

“Tunahimiza wanasiasa wanaotembelea makanisa yetu kuheshimu madhabahu. Wanasiasa watatakiwa kutulia na kufuatilia ibada hadi mwisho wa huduma. Hatutaruhusu siasa kanisani.

“Tutaombea mahitaji yao bila kuwapa fursa ya kuzungumza siasa kanisani. Kwa muda mrefu makanisa yamekuwa yakitumiwa na wanasiasa kuzua vurugu na kutoa matamshi ya uchochezi,” akasema Kasisi Mkuu Mutahi.

Kanisa hilo lilisema wanasiasa wanaofika katika makanisa ya PCEA kote nchini watatambulishwa na kisha kupungia mkono waumini na hawatapewa kipaza sauti kuzungumza. “Wanasiasa wanapokuja kanisani tunawahimiza kuwa sawa na waumini wengine.

Hii ni kwa sababu waumini wetu wanaegemea katika mirengo tofauti .”ya kisiasa hivyo hatutaki kuleta mgawanyiko kanisani,” akasema.

Kasisi Mkuu alisema kuwa marufuku hiyo inaanza kutekelezwa mara moja.Awaliwataka wanasiasa kuheshimu viongozi wa makanisa pamoja na waumini wanaoenda makanisani kuabudu.

Mutahi alisema marufuku hiyo inalenga kuzuia vurugu kama zilizotokea mwaka jana Dkt Ruto alipozuru Kanisa la African Independent Pentecostal Churches of Africa (AIPCA) katika Kaunti ya Murang’a.

Alisema alisema hatua hiyo inalenga kuepuka vurugu makanisani huku nchi ikijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

  • Tags

You can share this post!

Msongo wa mawazo unasababisha vijana kuota mvi mapema...

ODM yapuuza madai ya kupoteza ufuasi Pwani