• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
USWAHILINI: Posa asili ya Kidigo ilivyofanikishwa kwa kutumia washenga

USWAHILINI: Posa asili ya Kidigo ilivyofanikishwa kwa kutumia washenga

Na HAWA ALI

MVULANA wa Kidigo atokapo jandoni hutafutiwa mchumba.

Jambo la kwanza kufanyika ni kumtuma mshenga ili akaonane na nyanya wa msichana anayetakiwa kuposwa.

Mara nyingi, mshenga huwa babu, kaka, shemeji au mtu mwingine wa namna hiyo.

Mshenga hupeleka ada ya kwanza ya kuomba posa na kumpa nyanya wa msichana na kumweleza kuwa mjukuu wake ahitajiwa kuposwa.

Ada hii ilikuwa tumbaku au mapeni kadhaa. Baada ya hapo, nyanya alimjulisha mjukuu wake, kisha hutoa taarifa ya posa kwa wazazi wa binti.

Wazazi wakikubali, nyanya humpelekea habari mshenga kwamba posa imekubaliwa. Na hapo basi, mvulana hualikwa nyumbani kwa nyanya wa msichana ili amwone mchumba wake.

Kisha mshenga hupeleka ada ya kumpa msichana ambayo huitwa vilama nayo ni ushanga wa kuvaa shingoni au kiasi fulani cha sarafu lakini mara nyingi mapeni hayakuthaminiwa katika posa.

Baada ya ada hizo kutolewa, uchumba hukamilika kwa mvulana kutumwa kazi kadha wa kadha na wakweze.

Kazi ilikuwa mfano wa kufyeka msitu, kulima, kubeba mizigo na ujenzi. Kusudi lake hasa ni kujua iwapo mkwe wao anaweza kumtunza mke kwa kutumia nguvu zake mwenyewe.

Kitambi

Ada nyingine iliyotolewa wakati wa posa ni kitambi na kaniki.

Baba alipewa kitambi na mama kaniki.

Siku hizi baba hupewa kikoi na mama kitenge.

Mavazi haya ni mbadala wa kitambi na kaniki kutokana na sababu kuwa havitumiki siku hizi.

Ada nyingine ndogondogo hutolewa pia kwa watu wanaohusiana katika nasaba kama vile: mlezi, shangazi, nyanya na babu wa binti.

Hapo awali ada hizi zilikuwa vipimo maalum vya nafaka lakini kwa sasa hutolewa fedha. Baada ya ada hizi kutolewa ndoa hufungwa.

Mambo ya posa yalitofautiana kulingana na wakati. Hapo awali kidogo, ada za posa zilianza kutumika. Kwa mfano kulikuwa na barua ambayo ilifungwa kwa kitambaa na kukabidhiwa mjomba wa msichana.

Baada ya kupokea barua, mshenga alipangiwa siku ya kuchukua majibu.Siku hiyo ilipowadia, mchumbiaji na mshenga walikaa nje.

Mjomba wa mwari alitoka na kumchukua mchumbiwa ili akamwone mtu anayemchumbia.

Barua ilifungwa kwa kitambaa na kuandikwa mahari; yaani vitu vyote vilivyohitajika, kwa mfano baba hupewa kofia, kikoi, fulana na viatu.

Mama hupewa doti ya kitenge na shanga za shingoni. Bibi hupewa blanketi na kadhalika.

You can share this post!

Cherargei ataka DCI na EACC zichunguze matumizi mabaya ya...

Ataka mkataba kati ya viongozi Mlimani na wawaniaji Urais

T L