• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Precision Air: Mvuvi jasiri aliyekuwa mstari wa mbele kuokoa abiria apata kazi serikalini

Precision Air: Mvuvi jasiri aliyekuwa mstari wa mbele kuokoa abiria apata kazi serikalini

NA MARY WANGARI

MVUVI shujaa aliyekuwa sehemu ya kikosi cha watu waliookoa maisha ya abiria 24 wasliohusika kwenye ajali mbaya ya ndege ya shirika la Precision Air ametunukiwa kazi kwenye kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, ametoa amri hiyo leo Jumatatu, Novemba 7, 2022, kwamba Jackson Majaliwa aajiriwe kazi hiyo.

Akitangaza hatua hiyo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mvuvi huyo kijana ambaye tayari amezawadiwa Sh52,000 vilevile atapokea mafunzo ya ziada kuhusu operesheni za uokoaji ili kumpa ujuzi.

Waziri Mkuu huyo amesema haya wakati wa ibada maalum iliyoandaliwa kwa heshima ya abiria 19 walioangamia baada ya ndege ya Precision Air Nambari PW494 kutumbukia kwenye Ziwa Victoria mnamo Jumapili, Novemba 6, 2022.

“Rais Samia ameguswa na ujasiri wa kijana huyu na ameamuru Wizara ya Masuala ya Ndani kumpa kazi katika kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili apate mafunzo na ujuzi zaidi kuhusu operesheni za aina hiyo,” amesema Majaliwa.

“Ninamhimiza waziri atekeleze agizo hili upesi iwezekanavyo kwa kukusanya maelezo muhimu ya kijana huyu jasiri hatua nyinginezo zikifuata.”

Amesema serikali ya Tanzania imetambua juhudi za wavuvi wengineo waliohusika katika uokoaji huo akiahidi mipango kabambe ya kuboresha hali zao.

Majaliwa aliyekuwa mmoja kati ya watu wa kwanza kufika katika eneo ambapo ajali hiyo ilitokea, amesimulia jinsi alivyoponea kifo kwa tundu la sindano alipokuwa akijitahidi kuokoa maisha ya marubani waliokuwa wamekwama ndani ya ndege.

Alijeruhiwa katika harakati hizo na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kagera pamoja na abiria waliojeruhiwa akiwemo mfanyakazi katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba aliyezimia kutokana na mshtuko.

Aidha, Waziri Mkuu ametangaza kuwa serikali ya Tanzania itagharimia mazishi ya waliofariki kufuatia ajali hiyo huku akiagiza maafisa husika kufuatilia suala hilo.

[email protected]

You can share this post!

Youssoufa Moukoko aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao...

Mwanaharakati amshtaki Ruto kwa kufanya ubaguzi alipoteua...

T L