• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Ramaphosa afokea mataifa ya Afrika yanayotenga Afrika Kusini

Ramaphosa afokea mataifa ya Afrika yanayotenga Afrika Kusini

Na AFP

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

RAIS wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amelaani vikali nchi za Afrika ambazo zimepiga marufuku ndege kutoka taifa hilo, ambalo linakabiliwa na mkurupuko wa aina mpya ya virusi vya corona kwa jina Omicron.

Rais Ramaphosa alizitaka nchi za Afrika kukoma kuiga mataifa ya Magharibi, ambayo pia yamepiga marufuku ndege kutoka Afrika Kusini (SA) kama njia mojawapo ya kudhibiti msambao wa Omicron.

Mataifa ya Afrika ambayo yamefunga mipaka yake dhidi ya SA ni Rwanda, Ushelisheli, Morisi, Misri na Angola.

“Ninashangaa kwamba mataifa ya Afrika yamefuata nyayo za wakoloni (Magharibi) kuzuia ndege kutoka Afrika Kusini. Ninafahamu wana sababu zao, lakini ningependa nchi hizo ziache kufuata mataifa ya kigeni kwa kukimbilia kutenga Afrika Kusini bila ushahidi,” akasema Rais Ramaphosa muda mfupi kabla ya kuondoka SA kuzuru Afrika magharibi.

Miongoni mwa nchi ambazo zimepiga marufuku ndege kutoka Afrika Kusini duniani ni Uingereza, Amerika, nchi za Muungano wa Ulaya (EU), Japan, Uturuki, Ujerumani, Uholanzi, Brazil, Miliki za Uarabuni (UAE), Canada na Ufilipino.

Kenya, hata hivyo, imeshikilia kuwa haitachukua uamuzi huo.

Badala yake, serikali ya Kenya ilisema itaimarisha vipimo kwa wasafiri wanaoingia nchini kutoka Afrika Kusini na nchi jirani kama vile Namibia, Lesotho, Botswana, Eswatini na Zimbabwe, pamoja na mataifa ambayo yamethibitisha kuwa na virusi vya Omicron.

Virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini mnamo Novemba 24, na vimesambaa katika mataifa kadhaa.

SA imekuwa ikishutumu vikali nchi ambazo zimeiwekea vikwazo vya usafiri kufuatia ugunduzi huo.

Wanasayansi wanaendelea na majaribio kubaini ikiwa Omicron inaweza kupunguzwa makali na chanjo zilizopo kwa sasa.

SA inaendelea kutengwa huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likizitaka nchi kutumia mbinu mbadala za kuzuia msambao wa Omicron badala ya kuweka vikwazo vya usafiri.

WHO inapendekeza kuwa mataifa yanaweza kuwatia karantini wasafiri kutoka Afrika Kusini huku wakifanyiwa vipimo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema Jumatano kuwa marufuku dhidi ya ndege kutoka Afrika Kusini hayatazuia virusi hivyo kusambaa.

Kampuni ya BioNTech imeelezea matumaini yake kuwa chanjo inayotengeneza kwa ushirikiano na Pfizer inaweza ikatoa kinga imara dhidi ya Omicron.

Kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Omicron kimethibitishwa nchini Brazil.

Nchini Ujerumani, Kansela mtarajiwa Olaf Scholz amesema ataunga mkono pendekezo la kutoa chanjo ya lazima kwa kila mtu mwaka 2022, lakini wabunge watakuwa huru kupiga kura kulingana na hisia zao kuhusu suala hilo.

Wanasiasa Ujerumani sasa wanataka kuwekwe masharti makali zaidi ya kudhibiti virusi vya corona baada ya kiwango cha maambukizi cha siku saba zilizopita kuvunja rekodi.

You can share this post!

Wakulima sasa wauza mahindi yao nje ya nchi

Ronaldo aweka rekodi ya ufungaji mabao na kusaidia...

T L