• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Rudisha ajeruhiwa katika ajali ya barabarani Keroka

Rudisha ajeruhiwa katika ajali ya barabarani Keroka

RUTH MBULA Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mara mbili wa Olimpiki, Dunia na Afrika katika mbio za mita 800, David Rudisha anaendelea kupokea matibabu baada ya kuhusika katika ajali ya barabara iliyomsababishia majeraha madogo Jumapili.

Rudisha, 30, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio hizi za mizunguko miwili ya dakika 1:40.91 aliyoweka akishinda taji lake la kwanza la Olimpiki mwaka 2012 jijini London nchini Uingereza, alikuwa akiendesha gari lake la aina ya Toyota V8 mapema Jumapili.

Inasemekana gurudumu la gari hilo lilipasuka karibu na mji wa Keroka, Kaunti ya Kisii, na akagongana ana kwa ana na basi kutoka kampuni ya Ena.

Ajali yenyewe inasemekana kufanyika saa nne na nusu asubuhi katika barabara kuu ya Kisii-Keroka, ambayo inaorodheshwa kama mojawapo ya maeneo yaliyo na historia ya ajali nyingi za barabara.

Jirani mmoja wa bingwa huyu wa Riadha za Diamond League mwaka 2010 na 2011 ameambia Taifa Leo Dijitali kuwa mwanariadha huyo hayuko hatarini na amepata matibabu katika hospitali moja mjini Keroka kabla ya kuhamishiwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kilgoris katika kaunti ya Narok, anakotoka.

Ajali hii ilifanyika saa chache baada ya Rudisha kuchapisha ujumbe kwenye mtandao wake wa Twitter akisifu mama yake kwa kusema, “Nakupenda mamangu. Umekuwa baraka kwetu. Moyo wako wa ukarimu na utu hauna kifani. Mungu akubariki mwalimu.”

You can share this post!

BIASHARA YA UREMBO: Vipepeo wanavyovutia watalii Pwani

AKILIMALI: Ubunifu kupunguza gharama ya ufugaji samaki

adminleo