• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
Sabina Chege ajeruhiwa katika fujo zilizozuka Bungeni mnamo Alhamisi, Juni 8

Sabina Chege ajeruhiwa katika fujo zilizozuka Bungeni mnamo Alhamisi, Juni 8

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE Maalum Sabina Chege mnamo Alhamisi, Juni 8, 2023 alijeruhiwa katika fuja na rabsha zilizozuka Bungeni wakati wa kikao cha alasiri.

Wabunge walianza kupigana baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kudinda kuidhinisha hatua ya mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya kumtimua Bi Chege kama Naibu Kiranja wa Wachache na kumteua Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje katika nafasi hiyo.

Bw Wetang’ula alisema kuwa alichukua hatua hiyo baada ya mahakama moja ya Kiambu kutoa agizo la kusitishwa kwa mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa na wabunge wa Azimio kwenye mkutano wa kundi la wabunge wa muungano huo (PG) wiki jana.

Bi Chege ambaye ni Mbunge Maalum wa chama cha Jubilee, na ambaye ni miongoni mwa wabunge wa chama hicho ambao wameasi muungano huo na kuamua kuegemea mrengo wa Kenya Kwanza, aliumia mkono wa kushoto baada ya kudaiwa kugongwa na chupa na mbunge mwenzake wa kike.

Alifanyiwa huduma ya kwanza na wahudumu wa shirika la St John’s Ambulance kabla ya kukimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Wabunge wa Azimio walikasirishwa na uamuzi wa Spika Wetang’ula wakimkashifu kwa mapendeleo.

Juzi, kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi alikuwa amemuandikia barua Spika huyo akimjulisha kuhusu uamuzi wa Azimio kumwondoa Bi Chege na nafasi yake kupewa Bw Mwenje.

Lakini katika uamuzi wake, Spika Wetang’ula alisema kuwa hawezi kutekeleza mabadiliko hayo ya PG ya Azimio kufuatia agizo lililotolewa na mahakama ya Kiambu baada ya kesi kuwasilishwa huko kupinga kutimuliwa kwa Bi Chege.

“Nimetoa uamuzi kwamba Azimio imefuata taratibu zote hitajika na sipingi uamuzi wenu wa kumwondoa naibu kiranja wenu. Lakini kuna agizo la mahakama ambalo ni ajabu kwamba muungano wenu haufahamu. Ninashauri kwamba muombe mshirikishwe katika kesi hiyo,” Bw Wetang’ula akasema.

“Agizo hilo la mahakama limemtaja Spika na Bunge kama washtakiwa katika kesi hiyo inayopinga utaratibu wa kiusimamizi,” akaongeza.

Lakini baada ya Bw Wetang’ula kutoa uamuzi huo, fujo zilizuka bungeni hali iliyomlazimisha kuwafurusha wabunge saba kwa utovu wa nidhamu na kuchochea vurugu hizo.

Wabunge waliofurushwa ni Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Rosa Buyu (Kisumu Mjini Magharibi), T J Kajwang (Ruaraka ) na Bi Chege. Wote hao waliamriwa kutohudhuria vikao vya bunge kwa wiki mbili.

Fatuma Munyanzi (Malindi) na Catherine Omanyo (Mbunge Mwakilishi wa Busia ) nao walizimwa Bungeni kwa siku tano huku Mbunge Mwakilishi wa Machakos Joyce Kamene akiamriwa kutohudhuria vikao viwili.

“Wabunge hao miongoni mwa makosa mengine walikaidi uamuzi wa Spika, wakatoa matamshi ya yenye matusi, kushambulia mbunge mwenzao na kuonyesha mienendo ya kushusha heshima na hadhi ya Bunge hili,” akasema Bw Spika huku akizomewa na wabunge wa Azimio.

Baada ya hapo wabunge wa upinzani waliondoka Bungeni na kuhutubia kikao cha wanahabari ambapo walimlaani Bw Wetang’ula kwa kuchochea uasi ndani ya muungano huo na kudinda kuidhinisha kutimuliwa  kwa Bi Chege.

  • Tags

You can share this post!

Awali ilikuwa milio ya risasi na magaidi Lamu, sasa ni...

Gaucho afichua aliitunuka familia ya Raila nakala tatu za...

T L