• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
SADC sasa kupeleka kikosi DRC

SADC sasa kupeleka kikosi DRC

NA AFP

WINDHOEK, NAMIBIA

MATAIFA ya Kusini mwa Afrika yamekubali kupeleka wanajeshi kusaidia katika kukomesha mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako makundi ya wapiganaji yamekuwa yakiwahangaisha raia kwa miongo kadha.

Mkutano maalum wa Jumuiya ya Ustawi wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) ulikubaliana kwamba wanajeshi watumwe DRC “kulinda usalama na kurejesha amani.”

Mkutano huo ulihudhuriwa na marais wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kama vile Afrika Kusini, Angola na Tanzania. Rais Felix Tshisekedi wa DRC pia alihudhuria mkutano huo uliofanyika jijini Windhoek, Jumatatu.

Wengine waliokuwepo ni Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na mawaziri kadha kutoka mataifa wanachana wa SADC. Hata hivyo, taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo haikutaja idadi ya wanajeshi watakaotumwa DRC wala kutaja ni lini wanajeshi hao watatumwa.

Makundi ya wapiganaji yameendesha mapigano mashariki mwa DRC, kwenye utajiri wa madini, kwa muda wa miongo mitatu.

Kundi la M23, mojawapo ya makundi hayo, liliteka sehemu kubwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini, tangu lilipoanzisha tena mapigano mwishoni mwa 2021.

Mapigano hayo yamechangia zaidi ya watu milioni moja kutoroka makwao, kulingana na Afisi ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Ushirikishi wa Misaada ya Kibinadamu.

Baadhi ya wanajeshi kutoka mataifa matatu ya SADC—Afrika Kusini, Tanzania na Malawi- tayari wamekuwa wakiendesha shughuli za kiusalama mashariki mwa DRC tangu 2013.

Wanajeshi hao wamekuwa wakihudumu chini ya mwavuli wa kikosi cha UN cha kulinda amani nchini DRC, MONUSCO.

“Afrika Kusini iko tayari kuchangia katika kuimarishwa kwa wanajeshi wa kikanda ambao wanasaidia kuleta amani mashariki mwa DRC,” Rais Ramaphosa akasema kwenye taarifa.

Hatua ya mataifa ya SADC kutuma wanajeshi eneo hilo itapiga jeki wanajeshi wa mataifa wanachama wa mataifa ya Afrika Mashariki (EAC) ambao wamekomboa maeneo mengine yaliyodhibitiwa na wapiganaji wa M23 tangu Desemba 2022.

Lakini hadi wakati huu wanajeshi hao wameshindwa kuzima kabisa mapigano ya M23, hali ambayo imewakera wakazi wa DRC.

Kikosi cha wanajeshi wa EAC kinashirikisha wanajeshi kutoka mataifa ya Burundi, Kenya, Uganda na Sudan Kusini.

“Ipo haja kwa SADC kufanyakazi kwa pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki na makundi mengine ya kikanda ili kuimarisha juhudi zetu za kuisaidia serikali na watu wa DRC,” Rais wa Namibia Hage Geingob aliambia mkutano huo.

Naye katibu mkuu wa SADC Elias Magosi akasema: “Tumesikitishwa na kudorora kwa usalama mashariki mwa DRC kutokana na mapigano yanayotekelezwa na waasi wa M23 na makundi mengine ya wapiganaji.”

“Vita vilivyoendelea ndani ya mwaka mmoja uliopita vinahujumu uhuru na hadhi ya DRC pamoja na mipango yake ya maendeleo huku ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu Desemba 2023,” Magosi akaongeza.

Alisema hali hiyo inahitaji juhudi za pamoja za mataifa ya SADC na jumuiya zingine za kikanda “ili kurejesha amani na usalama nchini DRC.”

  • Tags

You can share this post!

Umma kuruhusiwa kuuona mwili wa shujaa Mukami Kimathi

Masaibu ya wazazi shule zikifunguliwa

T L