• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Samuel Eto’o kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Cameroon

Samuel Eto’o kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Cameroon

Na MASHIRIKA

MWANASOKA wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o atawania nafasi ya kuwa rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot).

Hii ni baada ya nyota huyo wa zamani wa Barcelona na Inter Milan kutangaza azma yake hiyo kupitia akaunti za mitandao yake ya kijamii akisema kinachomsukuma kufanya hivyo ni “mapenzi yake kwa Cameroon na utashi wake kwa soka”.

Uchaguzi wa urais wa Fecafoot uliocheleweshwa unatarajiwa kufanyika mnamo Disemba 11, 2021 kabla ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kuandaliwa nchini Cameroon kuanzia Januari 9, 2021.

Fecafoot haijatangaza tarehe ambapo itachapisha majina ya wawaniaji wote wa urais kwenye kinyang’anyiro hicho kijacho.

Eto’o, 40, alijivunia kipindi kizuri kitaaluma huku akishinda mataji kadhaa ya ligi na bara Ulaya akisakata soka ya kulipwa nchini Uhispania na Italia.

Mshindi huyo mara nne wa taji la Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Cameroon baada ya kupachika wavuni mabao 56 kutokana na mechi 118. Aliwahi pia kuhudumu kambini mwa Chelsea na Everton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa muda mfupi kabla ya kustaafu akipiga soka nchini Qatar

Katika kiwango cha soka ya kimataifa, alisaidia Cameroon kushinda taji la AFCON mnamo 2000 na 2002 pamoja na kuzoa nishani ya dhahabu kwenye Olimpiki za Sydney, Australia mnamo 2000.

Tangazo za Eto’o kuwania urais wa Facefoot linajiri siku kadhaa baada ya suitafahamu kuzuku kuhusu iwapo watu walio na uraia wa mataifa mawili wana uwezo wa kugombea kiti hicho. Eto’o alipata uraia wa Uhispania alipokuwa mchezaji wa Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Jules Denis Onana na Emmanuel Maboang Kessack ni wanasoka wengine wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon kuwahi kuwania urais wa Fecafoot. Wawaniaji wa kiti hicho katika uchaguzi ujao wana hadi Oktoba 11, 2021 kuwasilisha stakabadhi zao.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Polisi waanza kufanya uchunguzi baada ya moto kuchoma...

AKILIMALI: Magurudumu yanamvunia hela, ni kutia bidii tu!