• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Saratani adimu iliyokatiza maisha ya mwekezaji mashuhuri Lizzie Wanyoike

Saratani adimu iliyokatiza maisha ya mwekezaji mashuhuri Lizzie Wanyoike

Na MWANGI MUIRURI

SARATANI ambayo mnamo Januari 14, 2024 ilimuua mwekezaji mashuhuri Lizzie Muthoni Wanyoike huwa adimu kwa wanawake kwa kuwa ni ile ya mishipa ya kubebea mayai ya kushika uja uzito, yaani Fallopian tube cancer.

Bi Wanyoike atazikwa nyumbani kwake katika eneobunge la Gatanga Jumanne ijayo.

Saratani hiyo sanasana inasemekana huwaathiri wanawake ambao miaka imesonga (kati ya 50 kwenda juu) hasa baada ya kupoteza uwezo wa kupata damu yao ya kila mwezi.

Bi Wanyoike alikuwa na miaka 73 alipoaga dunia kutokana na makali ya saratani hiyo.

“Haijulikani ni kwa nini saratani hii huwavamia wanawake waliosonga kimiaka au baada ya kupoteza uwezo wa kupata hedhi. Hata ile kansa ya mfuko wa mayai ya mwanamke almaarufu ovarian cancer huaminika huwa imeanza katika mishipa hii ya fallopian,” akasema Dkt Leonard Gikera wa hospitali kuu ya Murang’a.

Alisema kwamba kansa hiyo sanasana huwaandama pia wasio na uwezo wa kushika mimba.

Kwa mujibu wa Dkt Inyathiu Kibe ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya viungo vya uzazi vya wanawake, dalili za saratani ya fallopian tube huwa fiche na ni vigumu kutambua uko nayo.

Alisema hiyo ndiyo hatari kuu ya saratani hiyo kwa kuwa hujiunda na kukua hadi kukomaa na wakati inakuja kutambuliwa, huwa imezidi viwango vya kuthibitiwa ikiwa imekuamulia mauti tu.

Hata hivyo, alisema dalili ambazo zinaweza zikaashiria kansa hiyo kuwa ndani ya mishipa hiyo ni pamoja na kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu kutoka uke, utambi usio wa kawaida na usio wa kutokana na ongezeko la uzani, uvimbe katika tumbo, maumivu ya tumbo, kuhisi presha bandia ya kwenda haja kubwa na ndogo, kuhisi hata baada ya kwenda haja kubwa na ndogo ni kama bado umebakisha cha ziada na pia kuvunja damu ambayo sio ya hedhi.

Iwapo mwaathiriwa atabahatika na kansa hiyo itambulike ikiwa haijasambaa sana, matibabu yanasemwa ni kupitia kuondoa eneo lililoathirika na hatimaye kuwekwa katika mpango maalum wa madawa na pia kuchomwa kwa miale ya UV.

Upasuaji ambao hutekelezwa huwa ni wa kuondoa mishipa hiyo pamoja na vitovu vyake vya mayai huku katika hali tata zaidi, ikihitajika kutoa hata chungu cha mwana.

Mwaathiriwa akishatibiwa, uwezo wake wa kuishi zaidi ya miaka mitano huwa mgumu.

Bi Wanyoike alitambuliwa kuwa na kansa hiyo mwaka wa 2020.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mbunge wa Gatundu Kaskazini abadilisha wimbo baada ya...

Waliopata kazi za mjengo watetea mradi wa ujenzi wa nyumba...

T L