• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Sebastien Migne ataja kikosi cha Harambee Stars

Sebastien Migne ataja kikosi cha Harambee Stars

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Sebastien Migne ametaja ‘Mswidi’ Christopher Mbamba na ‘Mwingereza’ David Sesay katika kikosi chake cha Harambee Stars cha wachezaji 24 kitakachotumika kwa mechi dhidi ya Black Stars ya Ghana ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwezi Juni/Julai mwaka 2019 nchini Misri.

Mbamba alizaliwa jijini Harare nchini Zimbabwe mnamo Aprili 30 mwaka 1992 babake akiwa kutoka Namibia na mamake Mkenya. Hata hivyo, amekuwa akiishi Uswidi na hata kuchezea timu ya taifa ya Uswidi ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17. Mshambuliaji huyu wa kati anachezea klabu ya Oskarshamns inayoshiriki ligi ya daraja ya tatu nchini Uswidi. Aliwahi kucheza soka yake nchini Norway na pia Uingereza kabla ya kurejea Uswidi.

Sesay, ambaye alizaliwa Septemba 18 mwaka 1998, ni beki wa pembeni kulia. Mzawa huyu wa Uingereza anashiriki ligi ya daraja ya nne nchini Uingereza katika klabu ya Crawley Town. Tetesi nchini Uingereza zinasema Sesay, ambaye bei yake inaaminika kuwa Sh46,514,787, anamezewa mate na West Bromwich Albion inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili. Hakuna habari kuhusu wazazi wa Sesay, ingawa jina hili linapatikana sana katika eneo la magharibi mwa Afrika.

Kwa jumla, Mfaransa Migne ametaja wachezaji 16 wanaosakata soka yao ya malipo nje ya Kenya wakiwemo Victor Wanyama (Uingereza), Michael Olunga (Japan), Erick Ouma (Uswidi), Musa Mohammed (Zambia), Brian Mandela (Afrika Kusini), Patrick Matasi (Ethiopia), Erick Johanna (Uswidi) na Masoud Juma (Libya).

Harambee Stars itaingia kambini Machi 17 jijini Nairobi kabla ya kusafiri nchini Ghana kumenyana na Black Stars mnamo Machi 23 mjini Accra. Kenya na Ghana tayari zimeshafuzu kushiriki AFCON 2019 nchini Misri na zitakuwa zikiwani kumaliza juu ya Kundi F angaa kupata kundi rahisi droo itakapofanywa mwezi Aprili. Majina makubwa yanayokosekana katika kikosi cha Migne ni mshambuliaji wa Zesco United nchini Zambia Jesse Were na beki Harun Shakava na mshambuliaji anayeshikilia rekodi ya kufungia Kenya mabao mengi Dennis Oliech wote kutoka Gor Mahia. Beki David ‘Cheche’ Ochieng’ pia hana hajaridhisha Migne kiasi cha kupata namba katika kikosi chake.

Kikosi cha Harambee Stars:

Makipa

Patrick Matasi (St Georges, Ethiopia), Farouk Shikalo (Bandari), John Oyemba (Kariobangi Sharks);

Mabeki

Erick Ouma (Vasalund, Uswidi), Musa Mohammed (Nkana, Zambia), David Owino (Zesco, Zambia), Brian Mandela (Maritzburg, Afrika Kusini), David Sesay (Crawley Town, Uingereza), Philemon Otieno (Gor Mahia), Benard Ochieng (Vihiga United), Joash Onyango (Gor Mahia);

Viungo

Erick Johanna (IF Brommapojkarna, Uswidi), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Ubelgiji), Ismael Gonzales (Las Palmas B, Uhispania), Paul Were (Trikala, Ugiriki), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, Uingereza), Francis Kahata (Gor Mahia), Christopher Tangen Mbamba (Oskarshamns, Uswidi), Dennis Odhiambo (Sofapaka), Anthony Akumu (Zesco, Zambia);

Washambuliaji

Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan), Duke Abuya (Kariobangi Sharks), Cliff Nyakeya (Mathare United), Masoud Juma (Al Nasr, Libya);

Wachezaji wa ziada

Abdallah Hassan (Bandari), Allan Wanga (Kakamega Homeboyz), Nicholas Kipkirui (Gor Mahia), Roy Okal (Mathare United), Cliffton Miheso (Club Olimpico Montijo, Ureno) 

  • Tags

You can share this post!

Rusty Gee: Anatumia muziki kukabili matumizi ya mihadarati,...

Gor Mahia kucheza Jumapili dhidi ya wenyeji Hussein Dey

adminleo