• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Sevilla wakomoa AS Roma kwa penalti na kunyanyua taji la Europa League

Sevilla wakomoa AS Roma kwa penalti na kunyanyua taji la Europa League

Na MASHIRIKA

SEVILLA walitia kibindoni taji lao la saba la Europa League mnamo Jumatano usiku baada ya kukomoa AS Roma ya kocha Jose Mourinho kwa penalti 4-1 baada ya kuambulia sare ya 1-1 ugani Puskas Arena jijini Budapest, Hungary.

Gonzalo Montiel aliyefunga penalti iliyoshindia Argentina Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa mnamo Disemba 2022 nchini Qatar, alirudia ubabe wake dhidi ya Roma.

Alipachika wavuni penalti ya ushindi baada ya Roger Ibanez na Gianluca Mancini kupoteza mikwaju yao.

Sevilla ambao ni miamba wa soka nchini Uhispania, sasa wameshinda fainali zote saba ambazo wamewahi kunogesha kwenye fainali ya Europa League. Nahodha wao, Jesus Navas, alikuwa sehemu ya kikosi kilichovunia Sevilla taji la kwanza la Europa League dhidi ya Middlesbrough mnamo 2006.

Ushindi wao dhidi ya Roma uliwapa tiketi ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2023-24 licha ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) nje ya mduara wa nne-bora mnamo 2022-23.

Roma, walionyanyua ubingwa wa Europa Conference League mnamo 2021-22, walishuka dimbani wakiwa na matarajio makubwa ya kutawazwa wafalme. Kocha wao, Mourinho, alikuwa akijivunia kushinda fainali zote tano za Europa League ambazo waajiri wake wa zamani waliwahi kunogesha.

Paulo Dybala wa Argentina aliwaweka Roma kifua mbele katika kipindi cha kwanza baada ya ushirikiano wake na Mancini kumwacha hoi kipa Yassine Bounou.

Hata hivyo, miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A), walitepetea katika kipindi cha pili cha mchuano huo ulioshuhudia wachezaji 14 na wakufunzi wawili, akiwemo Mourinho, wakionyeshwa kadi.

Sevilla walisawazisha mambo kuwa 1-1 kunako dakika ya 55 baada ya krosi ya Navas kumbabatiza Mancini na kushuhudia mpira ukijaa wavuni.

Roma, waliokuwa wameshinda fainali moja pekee kati ya nne za awali zilizoamuliwa kwa penalti, walionekana kubabaika na kuingiwa na mchecheto kabla ya penalti kupigwa. Kikosi hicho kilikuwa tayari kimewaondoa wafungaji wao matata wa penalti wakiwemo Dybala, Tammy Abraham na nahodha Lorenzo Pellegrini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Dalot arefusha mkataba wake kambini mwa Man-United hadi...

Sammy ‘Kempes’ Owino kuwania urais FKF

T L