• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Sharp Boys kujituma kutwaa ubingwa tena

Sharp Boys kujituma kutwaa ubingwa tena

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Sharp Boys kwa wasiozidi umri wa miaka 14 inasadiki kuwa inapania kujituma mithili ya mchwa kwenye mechi za Ligi ya KYSD 2019/2020.

Kocha wake, Boniface Kyalo anasema raundi hii hawana la ziada mbali wanalenga kubeba taji hilo kwa mara ya pili. Timu hiyo imeshiriki ngarambe hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2000. Anadokeza kuwa michuano ya msimu huu inapigiwa upatu kushuhudia msisimko wa kufa mtu kinyume na makala zilizopita.

”Nina imani vijana wangu wamekaa vinzuri kukabili wapinzani wetu na kuibuka mabingwa wa mechi za msimu huu,” anasema na kudai anafahamu silaha atakayotumia kukabili wapinzani wao.

Anakiri kwamba migarazano hiyo kamwe haitakuwa mteremko wala haitakuwa ‘tafadhali wacha tupenye’ mbali timu zote zimejipanga kuangaza wenzao dimbani. Katika mpango anasema shughuli zitakuwa noma zaidi maana timu itakayoshindwa kujipanga bila shaka itapangwa.

Kocha huyo anadai kuwa tayari timu sita zimeonyesha huenda zikaibuka moto wa kuotea mbali msimu huu. ”Bila kujipigia debe, Sharp Boys, Kinyago United, Young Achievers, Pro Soccer, MASA na Pumwani Foundation zinatazamiwa kupiga shughuli za kweli raundi hii,” alisema.

Mchezaji wa Sharp Boys, Abdi Karim Kalili atuzwa baada ya kuibuka mfungaji bora kwa kufuma mabao 30 kwenye Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 msimu uliyopita wa 2018/2019. Picha/ John Kimwere

Sharp Boys ni kati ya vikosi zilizojitwika jukumu muhimu la kukuza wanasoka chipukizi mashinani vile vile kuwapa mwongozo mwafaka ili kuibuka watu wa kutegemewa katika jamii. Sharp Boys imechangia pakubwa kuwapa mwelekeo zaidi ya chipukizi 100 katika mitaa ya Eastlands, Nairobi.

”Sharp Boys hutumia soka kuwaleta pamoja vijana chipukizi hasa kuwasadia kupiga chenga matendo maovu mitaani ikiwamo matumizi ya mihadarati kati ya mengine,” alisema na kuongeza kuwa juhudi zao zimesaidia wengi kupiga hatua kimasomo.

Anadai vijana tisa wachezaji wake tayari ni wanasoma vyuo vikuu mbali mbali pia zaidi ya wenzao 20 wasomi wa shule za sekondari tofauti nchini.

Kadhalika anasema Melvin Kamau ambaye ameajiriwa kama askari wa magereza alipitia mikononi mwake. Sharp Boys inajivunia kunoa makucha ya wachezaji wengi tu ambao huchezea vikosi tofauti ambavyo hushiriki mechi za Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Orodha yao inashirikisha: Tryon Omondi (Posta Rangers Youth), Bravin Omondi (Tusker Youth), Christopher Muriithi (Nunguni FC ya Machakos), Hussein Maina, William Okwasumi na Sudeis Hussein wote Uprising FC.

Uprising iliyokuwa inashiriki mechi za Nairobi East Regional League (NERL) tayari imefuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao.

Sharp Boys inajumuisha chipukizi hawa: Mohamed Ramadhan, David Mwangi, Wayne Orata (nahodha), Edward Njuguna, Carlos Odingo, Victor Mugambi, Simon Nzivo, Steve Mugambi, Eric Mutiso, Victor Aguya, Ayale Muktar, Joseph Orenga, Kevin Omondi na Hillary Busenei.

You can share this post!

Lionesses na Simbas zapanda viwango vya raga

Al-Shabaab watatu wauawa Kiunga

adminleo