• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Singapore kuwapa raia wake hela za bwerere

Singapore kuwapa raia wake hela za bwerere

Na LEONARD ONYANGO 

SINGAPORE, Singapore

KILA raia wa Singapore mwenye umri wa kuanzia miaka 21 na zaidi atapokea fedha za bwerere kati ya Sh10,000 na Sh30,000 kutoka kwa serikali, kulingana na waziri wa fedha.

Waziri Heng Swee Keat alisema serikali imeamua kuwapa raia wake fedha za bwerere baada ya kubainika kuwa bajeti ya mwaka huu ina fedha za ziada Sh760 bilioni ($7.6 bilioni) zisizokuwa na kazi.

Swee Keat alitoa tangazo hilo alipokuwa akisoma makadirio ya matumizi ya fedha katika bunge la nchi hiyo. Waziri huyo wa fedha alisema fedha hizo ni zawadi kwa raia wa Singapore.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa raia wa nchi hiyo wanafurahia matunda ya maendeleo, kulingana na shirika la habari la  Channel News Asia.

Serikali itagawa jumla ya Sh53.3 bilioni kwa raia wake.

Kiasi kitakachotolewa kitategemea mapato ya kila raia.  Raia wa mapato ya chini watapokea kiasi kikubwa huku mabwanyenye wakipata kidogo.

Waziri wa Fedha nchini Singapore Bw Heng Swee Keat. Amesema serikali imeamua kuwapa raia wake fedha za bwerere baada ya kubainika kuwa bajeti ya mwaka huu ina fedha za ziada Sh760 bilioni ($7.6 bilioni) zisizokuwa na kazi. Picha/ Hisani

Raia wenye mapato ya chini ya Sh2.8 milioni kwa mwaka watapewa Sh30,000 huku walio na kipato cha zaidi ya hapo watapokea Sh10,000.

Fedha hizo zitatolewa kwa raia wake kufikia mwishoni mwa 2018. Jumla ya watu milioni 2.7 wanatarajiwa kunufaika na fedha hizo.

Serikali ilikusanya fedha nyingi kutokana na ushuru kuliko kiasi kinachotakiwa kufanya miradi ya maendeleo katika mwaka wa matumizi ya fedha wa 2018/2019.

Kiasi cha fedha za ziada kitakachosalia kitatumiwa kufanyia shughuli nyinginezo. Heng alisema Sh500 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa reli.

 

Sh200 bilioni

Alisema Sh200 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuwasaidia raia wake kulipa gharama za mafuta na mpango wa bima unaolenga kuwasaidia wazee kujikimu kimaisha.

Kulingana na waziri wa fedha, uchumi wa Singapore unazidi kunawiri.

Alisema kando na fedha hizo za bwerere wananchi watapunguziwa ushuru. Baaadhi ya huduma zitakazopata punguzo la ushuru ni ununuzi wa nyumba, karo ya wanafunzi.

Kwa mfano, mtu anayetaka kununulia familia yake nyumba ya kuishi, serikali itamwongezea Sh1.5 milioni. Awali walikuwa wakipokea Sh1 milioni lakini kiasi hicho kimeongezwa kwa asilimia 50.

Idadi kubwa ya raia wa Singapore ni wazee wa zaidi ya miaka 65. Watoto wanaozaliwa kila mwaka ni chini wastani wa kimataifa. Sheria kali kuhusiana na uhamiaji pia zimechangia katika kupungua kwa idadi ya watu.

You can share this post!

Naogopa kusimama kizimbani katika mahakama za Kenya, raia...

Riba ya ‘Okoa Jahazi’ ya Safaricom ni haramu,...

adminleo