• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
Sonko aacha Kalonzo mataani, ajiunga na Ruto

Sonko aacha Kalonzo mataani, ajiunga na Ruto

WINNIE ATIENO Na JURGEN NAMBEKA

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi Bw Mike Sonko amejiunga na muungano wa Kenya Kwanza wake Naibu Rais Wiliam Ruto baada ya azma yake ya kugombea kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa kuzimwa.

Bw Sonko alikuwa akitumia tikiti ya chama cha Wiper ambacho ni chama tanzu katika Azimio la Umoja One Kenya lakini juhudi zake zikagonga mwamba.

Mnamo Jumamosi, alikutana na mgombea urais wa muungano wa Kenya Kwanza Naibu Rais William Ruto na kutangaza kuwa amehama kutoka Azimio.

Bw Sonko alidai kwamba, aliahidiwa nafasi saba katika serikali kuu na nyingine katika serikali za kaunti za Nairobi na Mombasa iwapo Dkt Ruto atashinda urais.

Bw Sonko aliyemezea mate ugavana wa Mombasa alitangaza kuwa ametupilia mbali azima yake na kumuunga mkono Dkt Ruto.

Masaibu ya Bw Sonko yalianza mnamo 2020 alipobanduliwa kama gavana wa Nairobi mnamo 2020 kwa madai ya matumizi mabaya ya afisi yake na ufisadi.

Siku mbili zilizopita, jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu lilitupilia mbali ombi lake la kutaka uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wa kufutilia mbali kuidhinishwa kwake kama mgombea wa kiti cha Ugavana utupiliwe mbali.

Bw Sonko aliyekuwa akigombea kiti hicho na mgombea mwenza wake Bw Ali Mbogo, ameamua kumuunga mkono mwaniaji ugavana kaunti ya Mombasa kwa chama cha UDA Bw Hassan Omar pamoja na mgombea wa ugavana kaunti ya Nairobi kwa tiketi ya chama hicho Bw Johnson Sakaja.

Bw Sonko alidai ameahidiwa nafasi ya waziri katika serikali ya Kenya Kwanza, nafasi mbili za makatibu wa wizara, na nne za mabalozi katika makubaliano aliyotia saini na Dkt Ruto.

Katika serikali ya kaunti ya Mombasa, Bw Sonko ameahidiwa kuwa atapewa nafasi tatu za mawaziri. Katika kaunti ya Nairobi atapewa nafasi mbili za mawaziri na maafisa watatu wakuu.

“Mnajua yale ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda. Nimesukumwa kabisa katika nia yangu ya kuwapigania watu wa Mombasa. Kama kiongozi, lazima niungane na viongozi ambao wana maono mazuri kwa ajili ya watu wangu,” alisema katika mtandao wake wa kijamii baada ya Dkt Ruto kumkaribisha katika mrengo wake.

Alieleza kuwa, aliamua kushirikiana na Dkt Ruto kwa sababu ya maisha ya siku za usoni ya watu wa Mombasa.

“Sitamwacha ndugu yangu Bw Mbogo nyuma kwa kuwa amekuwa nami katika changamoto hizi. Kwa hivyo, zile nyadhifa nilizopewa lazima nimkumbuke. Nafanya hivi ili watu wangu wapate nafasi za kazi katika kaunti za Mombasa na Nairobi,” alisema Bw Sonko.

Hata hivyo haikubainika msingi ambao atatengewa nyadhifa hizo ikizingatiwa sio kiongozi wa chama na kutokana na uamuzi wa mahakama, hawezi kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa kuwa aliondolewa ofisini kwa kutumia vibaya mamlaka yake.

Bw Sonko alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka kwa kusimama naye.

Alieleza kuwa Rais Kenyatta amekuwa kama ndugu.

  • Tags

You can share this post!

Mashirika, viongozi wa kidini wataka IEBC kuzingatia...

DINI: Mstari kati ya wema na ubaya ni mwembamba

T L