• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Sudan: Amerika yatishia kuweka vikwazo vipya

Sudan: Amerika yatishia kuweka vikwazo vipya

NA MASHIRIKA

WASHINGTON DC, AMERIKA

RAIS wa Amerika Joe Biden amesema mzozo wa Sudan unapaswa kudhibitiwa huku akitishia kuweka vikwazo vipya dhidi ya viongozi wanaounga mkono mapigano hayo.

Hii ni baada ya rais huyo kutia saini amri ya rais inayompa mamlaka ya kuwawekea vikwazo wahusika wanaotishia amani, usalama na utulivu wa Sudan pamoja na kudhoofisha mchakato wa mpito kwa njia ya demokrasia. Hata hivyo taarifa ya Biden haikuwataja walengwa.

Rais Biden amesema mapigano yanayoendelea ni usaliti wa matakwa ya watu wa Sudan ya kupatikana kwa serikali ya kiraia na mpito wa kidemokrasia. Matamshi hayo yametolewa kutokana na hatua ya pande zote mbili zinazozozana Sudan, kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku saba, baada ya mashambulio ya angani na makombora kushuhudiwa kwenye mji mkuu, Khartoum.

Biden, aidha amezitaka pande zinazohusika kukomesha mapigano.

Amesema mapigano nchini Sudan ni janga na usaliti dhidi ya watu wa taifa hilo , wanaotaka serikali ya kiraia na mpito wa kidemokrasia na kusisitiza machafuko ni lazima yakomeshwe.

Mamia ya watu tayari wamekufa kwenye mapigano yaliyozuka Aprili 15 kati ya jeshi la serikali linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na aliyekuwa makamu wake, Hamdan Daglo wa Vikosi vya Dharura, RSF.

Katika mji mkuu Khartoum, mapigano yaliendelea kushuhudiwa Alhamisi na kuvuruga kabisa juhudi za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa.

Huku hayo yakiendelea, taarifa kutoka Geneva, zimesema Shirika la Chakula Duniani (WFP), limepoteza bidhaa zenye thamani ya kati ya Sh1.7 bilioni zilizopaswa kupelekwa Sudan, tangu kuzuka kwa mapigano hayo.

Mkurugenzi wa WFP nchini humo, Eddie Rowe, alisema bado wanatayarisha taarifa kuhusu wizi wa bidhaa hizo huku akielezea kukithiri kwa wizi nchini humo. Alieleza kuwa kila uchao wanaarifiwa kuhusu wizi wa bidhaa hizo.

Rowe alitoa taarifa hizo, siku moja baada ya mkuu wa huduma za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths, kutoa wito kwa pande zinazozozana nchini Sudan kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapata misaada.

Haya yamejiri siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuhimiza mapigano Sudan yasitishwe.

Kwa upande mwingine, alitoa wito pande zote mbili zinazozozana kuheshimu maafisa wanaotoa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa.

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri mwingine Kilifi naye atiwa mbaroni sababu msichana...

DOUGLAS MUTUA: Uhusiano wa Urusi na Afrika utawaramba...

T L