• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Sukari: Kamati yaambiwa wabunge 2 walipelelezwa na DCI

Sukari: Kamati yaambiwa wabunge 2 walipelelezwa na DCI

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kiambaa Njuguna Ka Wanjiku na mwenzake wa Thika Mjini Alice Ng’ang’a walihojiwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusiana na kutoweka kwa magunia 20,064 ya sukari yenye sumu katika bohari moja mjini Thika.

Mkurugenzi wa kampuni ya Vinepark Ltd inayomiliki bohari hilo Peter Mwangi mnamo Julai 21, 2023, aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Biashara kwamba alikamatwa mnamo Mei 3, na maafisa wa DCI na kupelekwa katika hoteli ya Panafric ambako aliwapata wabunge hao wawili wakihojiwa na maafisa hao.

“Niliwapata wanasiasa hao wawili wakihojiwa. Mheshimiwa Ka Wanjiku aliulizwa kwa nini alikuwa akinipigia simu,” Bw Mwangi akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Biashara James Gakuya (kulia) akiongoza kikao cha uchunguzi kuhusu sakata ya kutoweka kwa sukari yenye sumu kutoka bohari moja mjini Thika Mei 2023. Kushoto ni Naibu mwenyekiti wa Kamati hiyo Maryanne Keitany, Mbunge wa Aldai. PICHA | CHARLES WASONGA

Hakuelezea ni kwa nini Bi Ng’ang’a alikuwa akihojiwa akisema “polisi siku hizi huwakamata watu waliokupigia simu baada ya kutwaliwa kwa simu baada ya kukamatwa kwako.”

Bw Mwangi alisema baada ya kuhojiwa kwa dakika 35 katika mkahawa huo, aliwekwa nyuma ya gari aina ya Subaru na kupelekwa katika makao makuu ya DCI.

Alimpata mwanamume kwa jina Mohammed na kwa pamoja walihojiwa na kisha kupigwa.

Bw Mwangi alisema Mohammed alikamatwa baada ya kubainika kuwa alimpigia simu mara kadha baada na kabla ya kukamatwa kwake.

“Bw Mohammed alikuwa amenitumia ujumbe wa WhatsApp akinionya kuwa sukari ilikuwa imeibwa kutoka kwa ghala la kampuni ya Kings Community ambalo nilikuwa nimekodisha kuhifadhi bidhaa hiyo,” Bw Mwangi akawaambia wabunge wanachama wa kamati hiyo ambayo imekuwa ikiendesha uchunguzi kuhusu kupotea kwa sukari hiyo ya thamani ya Sh200 milioni na iliyosafirishwa kutoka Mombasa.

Bw Mwangi aliwaambia wabunge hao kwamba Bw Mohammed alimwambia kwamba baada ya sukari hiyo kuondolewa kutoka ghala hilo la Thika ilisafirishwa hadi Mombasa kuuzwa.

“Aliniambia wakati tulikuwa tumekamatwa kwamba sukari ambayo ilikuwa imetolewa kutoka bohari la Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) mjini Mombasa na kusafirishwa hadi Thika baadaye ilirejeshwa kuuzwa Mombasa ili kuificha,” Bw Mwangi akasema.

“Ama kwa hakika tulipokuwa tukihojiwa Mombasa, Bw Mohammed alipelekwa mahali fulani na akarejea na magunia 12 ya sukari yenye sumu. Magunia hayo ya sukari hiyo ilikuwa na vibandiko vilivyofanana na magunia ya sukari yaliyokuwa yamehifadhiwa katika ghala la Thika,” Bw Mwangi akaongeza.

Kamati ya Bw Gakuya imekuwa ikichunguza wizi wa sukari hiyo ambayo ilikuwa imetolewa kwa kampuni ya Vinepark Ltd ili itumiwe kutengeneza kemikali inayojulikana kama “ethanol” ya kutumika viwandani.

Bw Mwangi aliwaambia wabunge kwamba maafisa sita wa KRA walikuwa wamefunga bohari hilo hata kabla ya kubaini ikiwa masharti yaliyowekwa ya kusafirisha na kuharibu sukari hiyo yalitimizwa.

Mnamo Mei 3, 2023, maafisa wa KRA walirejea katika bohari hilo wakiongozwa na Faith Kuria kulifungua ili kuthibitisha kuwa sukari hiyo ilikuwepo.

“Kufuli zilipovunjwa na stoo kufunguliwa, hakukuwa na chochote. Naamini kuwa kulikuwa na njama ya kuondoa sukari hiyo kisiri,” Bw Mwangi akasema.

Hata hivyo, Bi Pamela Ahego ambaye ni Kamishna wa KRA anayesimamia forodha na udhibiti wa mipaka, ambaye alifika mbele ya kamati hiyo aliiondolea lawama asasi hiyo.

Alisema wajibu wa KRA ulikamilika ilipowasilisha sukari hiyi kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) na Shirika la Kukagua Ubora wa Bidhaa (KEBS) katika bohari lilikodiwa na kampuni ya Vinapack.

“Kontena zilizobeba sukari hiyo zilipowasilishwa katika bohari chini ya usimamizi wa kampuni ya Vinepack, Nema na Kebs mjini Thika, vibandiko vya kielektroniki viliondolewa. Bidhaa hizo sasa zilikuwa tayari kutumiwa kutengeneza ‘ethanol’,” akasema Bi Ahego.

“Baada ya hilo kufanyika, wajibu wetu ulikamilika hapo,” Kamishna huyo akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo ajitokeza hadharani baada ya kutoonekana wakati wa...

Uhuru alivyofaulu kukwepa ‘mtego’ wa polisi Karen

T L