• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Sum apata ushindi wa pili mfululizo nchini Uswizi

Sum apata ushindi wa pili mfululizo nchini Uswizi

Na GEOFFREY ANENE

EUNICE Sum ameonyesha kupata makali yaliyomfanya kuibuka malkia wa mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia (2013) na Jumuiya ya Madola na Afrika (2014) alipoandikisha ushindi wa pili mfululizo nchini Uswizi mnamo Agosti 1, 2019.

Sum, ambaye alitwaa taji la duru ya Riadha za Diamond League mjini Zurich nchini Uswizi mnamo Agosti 29 kwa dakika 2:00.40, aliibuka mshindi wa shindano la Gala dei Castelli mjini Bellinzona nchini humo kwa dakika 2:00.94.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 31 alibwaga wapinzani wake wa karibu, Waswizi Lore Hoffmann, 23, (2: 01.90), bingwa wa mbio za mita 800 za bara Ulaya za Ukumbini Selina Buchel (2: 02.61) na mshindi wa nishani ya shaba ya Riadha za Dunia za Under-20 Delia Sclabas (2: 04.16).

Sum anatarajiwa kurejea nyumbani kutafuta tiketi ya kushiriki Riadha za Dunia katika mchujo wa kitaifa utakaofanyika katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo mnamo Septemba 3.

Muda wake dakika 2:00.40 ni ndani ya muda unaohitajika kufuzu kushiriki Riadha za Dunia za mwaka huu wa 2:00.60. Hata hivyo, huenda ikawa lazima kwake kushiriki mchujo huo ili kujihakikishia tiketi ya Riadha za Dunia kwa kumaliza katika nafasi tatu za kwanza.

Wanariadha kutoka Kenya walio katika viwango bora vya mbio za mita 800 za wanawake mwaka huu ni Emily Tuei (nambari 21 duniani), Sum (37), Jarinter Mwasya (55), Eglay Nalyanya (71) na Jackline Wambui (86) ambao pia wanatarajiwa kutifua vumbi kuwania tiketi.

Sum ndiye Mkenya wa mwisho kushinda medali katika mbio hizi za mizunguko miwili za kinadada kwenye Riadha za Dunia aliponyakua shaba mwaka 2015 mjini Beijing nchini Uchina.

Kenya tayari imeshachagua wawakilishi wake wa mbio za mita 10,000 na kilomita 42. Itakuwa ikichagua wawakilishi wa vitengo hivyo vingine Septemba 3. Riadha za Dunia zitafanyika Septemba 27 hadi Oktoba 6, 2019 jijini Doha nchini Qatar.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Simbas yashuka viwango bora vya raga duniani

Kinyago yazikaranga MASA na Fearless bila uoga

adminleo