• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Tabitha Karanja ajiunga na UDA

Tabitha Karanja ajiunga na UDA

Na WANGU KANURI

MFANYABIASHARA Tabitha Karanja ambaye alikuwa ametangaza azma yake ya kuwa kuwania kiti cha useneta katika kaunti ya Nakuru, amejiunga na chama cha United Democratic Party (UDA).

Bi Karanja alikaribishwa kwenye chama hicho na Naibu Rais William Ruto aliyekuwa amepeleka kampeni zake kwenye kaunti hiyo.

“Si huyu ni mtu wa Bottom-Up? Si ameanza hapa chini? Mngependa kumuona akifanya kazi nami, na Moses Wetangula, Musalia Mudavadi, Nderitu Gachagua, Ndindi Nyoro na Susan Kihika?” Dkt Ruto akauliza umma uliomiminika katika uwanja wa Nakuru.

Akizungumza kabla hajavishwa kofia ya UDA, ishara amejiunga na chama hicho, Bi Karanja ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kutengeneza pombe na mvinyo ya Keroche, aliwaahidi wakazi wa Nakuru kuwa lengo lake akichaguliwa, ni kuhakikisha kuwa sheria zinazotungwa serikalini haziwanyanyasi.

“Shida ambayo sisi wanabiashara tumepitia ni mingi na tungependa mazingira mema ili biashara zikue nchini. Utozwaji wa juu wa ushuru pia umechangia katika kusambaratisha biashara na tungependa Dkt Ruto uhakikishe kuwa utafuata kauli ya Buy Kenya, Build Kenya kikamilifu,” akaongeza.

Bi Karanja ananuia kumrithi Susan Kihika ambaye hivi sasa ndiye seneta wa kaunti hiyo. Bi Kihika naye amelenga kuwania kiti cha ugavana cha kaunti hiyo na kumrithi Lee Kinyanjui ambaye anaegemea mrengo wa vuguvugu la Azimio la Umoja linaloongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mkutano huo wa hadhara ulikuwa wa kwanza tangu Dkt Ruto kuahidi kushirikiana na kiongozi wa chama cha Amani National Congress, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wa chama cha Ford-Kenya.

You can share this post!

Akana kuiba Bibilia tatu

AFCON: Morocco kukutana ama na Misri au Ivory Coast kwenye...

T L