• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
TALANTA: 4K Club ya aina yake

TALANTA: 4K Club ya aina yake

NA PATRICK KILAVUKA

KUSTAWISHWA kwa klabu ya Kilimo mwaka jana katika shule ya msingi ya Muguga Green, kaunti ndogo ya Westlands, Kaunti ya Nairobi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza kurejelewa kwa klabu ya 4K CLUB, kulikuwa jukwaa murua la kuinua vipawa vya wanafunzi ambao walikuwa na kiu kubwa ya kupata maarifa ya kilimo hususan katika kilimo mseto yaani ufugaji na ukuzaji mimea.

Wanafunzi zaidi ya 60 wamepata fursa ya kujifunza jinsi ya kupanda mboga kama sukumawiki, kabeji, spinachi, nyanya, vitunguu na hata ndizi.

Aidha, wamejifunza pia kufuga wanyama kama mbuzi na kuku.

Haya yote wanayafanya kwa uelekezi wa mwalimu wa somo la Kilimo Theophilus Muoki ambaye huwafunza darasani na kufanya zoezi la nyanjani.

Shule pia imewakumbatia kwa udhamini wa mbegu na vyakula vya kulisha kuku na mbuzi pamoja na kuhakikisha kuna maji ya kutosha kwa kilimo cha unyunyiziaji mimea.

Mtaala wa umilisi umekuwa mhimili muhimu sana kwa klabu hii shuleni kwani, wengi wa wanachama wa klabu ni wanafunzi wa gredi ya tano na sita.

Katika upanzi, wanaklabu hawa huhakikisha wanapanda katika misimu ambayo wanapata maji kutokana na mvua kama njia ya kupunguza utumizi wa maji ya mifereji kwa sababu ya gharama ya ada za maji. Wao hupanda mboga zao haswa katika miezi ya Machi na Novemba.

Wanasema kilimo chao hunawiri sana mwezi wa Aprili na hupata mavuno mazuri.

Kilimo mseto kimewawezesha wanafunzi hawa kujifunza mambo mengi.

Hususan kimechochea vipaji vyao vya ukulima huku wengi wao wakikariri kwamba, kilimo kikiwa uti wa mgongo wa taifa letu, watakuwa wakulima siku za usoni kwani kuna dhahabu ambayo imefichwa ndani ya udongo na mifugo.

Wameweza kujitambua katika fani ya kilimo kwani kadri wanavyozidi kujitanua katika kilimo, ndivyo ari yao inazidi kukua.

Manufaa ambayo wamevuna kutokana na klabu hii ni kwamba, wengi wao kwa sasa wanaazimia kujiendeleza kupitia kilimo wakiamini kuwa, kupanda mboga kunaweza kuwapa hela za haraka kwa muda mfupi, chakula cha kutosha, nyama ya mifugo na kuku pamoja na mayai. Hivi hasa ndivyo vigezo muhimu vya lishe bora.

Wanaamini kilimo kikiimarishwa, taifa litakuwa na afya bora. Wanachama wako tayari kuhudumia nchi katika nyanja mbalimbali na kupunguza uwezekano wa magonjwa kutamalaki.

Mbali na kilimo kuwa njia ya mapato na ajira, mapato ya klabu hii husaidia baadhi ya wanachama kukimu matakwa ya kimsingi kwa wale wanaotoka katika jamii zenye changamoto kama kuwanunulia vitabu na kalamu.

Wanaklabu huchangia katika kupanda na kunyunyizia mimea maji na dawa, kulisha kuku na kadhalika.

Isitoshe, wametia fora katika mazoezi ya kilimo na wana uwezo wa kutunza wanyama na kupalilia na kunyunyuzia maji mboga na kutunza mazingira.

Mbali na kutambua jinsi ya kukabiliana na magonjwa ambayo huathiri mboga na wanyama, wanashauri kwamba kilimo ni chanzo cha utajiri wa taifa.

Asasi za kilimo zinafaa kuwapa wakulima vifaa vya kilimo mfano; mbegu na mbolea kwa bei nafuu ili kuinua mazao ndipo taifa lijitegemee katika utoshelevu wa chakula.

You can share this post!

Mafuriko yaua watu zaidi nchini Pakistan

PAUKWA: Ulevi wa Magongo wamtosa mocharini

T L