• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Taliban wawapa wanajeshi wa Amerika siku 7 waondoke

Taliban wawapa wanajeshi wa Amerika siku 7 waondoke

Na MASHIRIKA

KABUL, AFGHANISTAN

WAPIGANAJI wa Taliban wameonya kuwa wanajeshi wa Amerika wataona cha mtema kuni iwapo wataendelea kuwa nchini Afghanistan kuanzia Septemba.

Msemaji wa Taliban, Suhail Shaheen, Jumatatu alisema kuwa kundi hilo halitaruhusu wanajeshi wa Amerika kuendelea kuwa humo nchini kuanzia Septemba 1, 2021.

Shaheen alisema waliafikiana na Rais wa Amerika, Joe Biden kuwa wanajeshi wake wataondoka nchini Afghanistan kufikia Agosti 31 wala hawatawaongezewa muda.

Amerika ilituma majeshi yake nchini Afghanistan ili kusaidia katika juhudi za kuokoa washirika wake baada ya kundi la Taliban kupindua serikali ya Rais Ashraf Ghani ambaye sasa anaishi uhamishoni katika Milki za Uarabuni (UAE).

“Rais Biden alisema kuwa wanajeshi wake wataondoka nchini Afghanistan kufikia Agosti 31. Iwapo hawatakuwa wameondoka kufikia wakati huo tutawachukulia kama wavamizi na tutakabiliana nao,” akasema Shaheen.

Taliban ilitoa onyo hilo, huku Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson akilenga kutumia mkutano wa leo Jumanne, wa mataifa tajiri zaidi duniani (G7), kumsihi Rais Biden kutoondoa majeshi ya Amerika nchini Afghanistan baada ya Agosti 31.

Johnson alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya watu wanaotaka kuondoka Afghanistan wanasaidiwa kutoka.

Maelfu ya Waafghanistan na raia wa kigeni wangali wamejazana katika uwanja wa ndege wa Kabul wakitaka kutoroka nchi hiyo.

Inakadiriwa kuwa jumla ya watu milioni 2.2 wamejaribu kutoroka Afghanistan. Takribani watu milioni 3.5 tayari wametafuta hifadhi katika nchi jirani kwa kuhofia utawala wa kundi la Taliban.

Waziri wa Ulinzi wa Amerika Lloyd Austin aameagiza mashirika ya ndege ya nchi hiyo kutoa ndege 18 zitakazotumiwa katika juhudi za kuokoa watu kutoka Afghanistan.

Mashirika ya ndege ya Atlas Air, Delta Air Lines na Omni Air yatatoa ndege tatu kila moja.

Kampuni ya Hawaiian Airlines itatoa ndege mbili na United Airlines itatoa ndege nne.

Ndege hizo zitatumiwa kuokoa watu walio nje ya mji wa Kabul.Wakati huo huo, Shaheen alisema wapiganaji wa Taliban tayari wamezingira mkoa wa Panjshir.

Mkoa huo ndio wa pekee ambao haujawa chini ya udhibiti wa Taliban.

Kundi hilo linadhibiti mikoa 33 kati ya 34.

Alisema kuwa wapiganaji wa Taliban tayari wamedhibiti wilaya za Pul-e-Hisar, Deh Salah na Banu.Makamu wa kwanza wa Rais Amrullah Saleh na maafisa kadhaa wa iliyopinduliwa wamejificha katika mkoa wa Panjshir.

You can share this post!

Hasara kuu kongamano la magavana likifutiliwa mbali

Walimu wakosa chanjo ya corona kituoni