• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
Teknolojia inavyowasaidia chipukizi kufanya mazoezi

Teknolojia inavyowasaidia chipukizi kufanya mazoezi

NA RICHARD MAOSI

Licha ya maambukizi ya Covid-19 kulemaza jumuiya ya wapenzi wa soka, ni wakati ambapo huenda teknolojia ikaawafaa wachezaji wanaojifanyia mazoezi bila kufuatiliwa na wakufunzi.

Wajibidiishe kuweka juhudi ili kubakia katika fomu nzuri ya mchezo msimu ujao, licha ya ukosefu wa wafadhili katika kandanda mashinani na kwa timu nyingi zinazoshiriki KPL nchini.

Hali ni kama hiyo kwa timu ya Nakuru Youth Sports Association ya wachezaji wasiozidi miaka 13, ambao wanajaribu kuweka nguvu zao katika soka.

Mkufunzi Mildred Ayanda ametengeneza kundi la Watsaap, ukumbi ambao anatumia kuwaleta pamoja wachezaji, usimamizi wa timu na wazazi.

Hii ni katika kampeni ya kutii agizo la serikali la kudumisha umbali wa zaidi ya mita moja kuzuia usambaaji wa Covid-19.

Kila mara wanapoingia uwanjani wao huhakikisha wamebeba mabango yanayoashiria nyenzo za kudumisha afya kama vile kuvalia barakoa.

Kikosi cha Nakuru Youth Spotts Association kinajumuisha wachezaji baina ya miaka saba hadi 13s wote wakijaza nafasi ya kwanza wakati wa michuano ya kiraki na FKF tawi la Magharibi ukanda wa kati.

Angel Muthoni nahodha wa timu ya akina dada anasema mbali na kusoma anapenda kucheza soka na marafiki zake.

Akiwa na umri wa miaka saba anasema tangu janga la Covid -19 kubisha amelazimika kufuata masharti ya mkufunzi wao kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsAap kufanya mazoezi ya kibinafsi.

Chini ya uangalizi wa wazazi wake mara tatu kwa wiki anaweza kutenga saa moja hivi kunyoosha viungo vya mwili mbali na kujiongezea ujuzi wa mpira.

Muthoni ambaye ni mwanafunzi wa Kariba Primay School mjini Nakuru anatarajia kwamba hivi karibuni hali ya kawaida itarejea ili yeye pamoja na wachezaji wenzake warejee uwanjani kusakata kabumbu.

Aidha angependa kuwashauri wachezaji wenzake kote nchini kuzingatia nidhamu na masharti ya serikali ili kujikinga dhidi ya maradhi ya Corona.

“Ninaamini kuwa tukiyafuata masharti ya serikali kama vile kunawa mikono na kuvalia maski tutashinda virusi hatari vya Covid-19,”akasema.

Kwa upande mwingine Joe Wyne mwenye umri wa miaka tisa anakubaliana na mawazo ya Angel kwa asilimia kubwa.

Anasema alianza kucheza soka akiwa na miaka sita na amekuwa akiendeleza taaluma yake kwa miaka mitatu sasa.

Siku za usoni analenga kucheza soka kama taaluma yake, pia anapendelea kusakatia timu ya Gor Mahia na Manchester City ya Uingereza.

Kulingana na Wyne ingawa Covid-19 imeharibu mpangilio wa ratiba ya michezo kote duniani bado hajakata tamaa na anaamini kuwa bado ataendelea kucheza soka.

“Ninapenda kucheza mpira kwani soka hunisaidia kuweka hali ya juu ya nidhamu mbali na kunisaidia kukua kimawazo na kiafya,”akasema.

Anapenda kucheza mpira msimu wa likizo akiwa mshambulizi matata, lakini sasa hali imebadilika ikimlazimu kufuatilia soka ya kimataifa kupitia mtandao wa kijamii.

Mara nyingine anapata maagizo kupitia simu ya mzazi wake ili kujipiga msasa na kwa mara ya kwanza anakubali kuwa teknolojia itamfaa pamoja na wenzake katika kipindi hiki kigumu.

Kwa sababu hakuna mazoezi mkufunzi Mildred anasema yeye hulazimika kuwapigia wazazi simu ili kuwasaidia watoto wao waweze kufanya mazoezi ya kibinafsi.

Anawahimiza kutenga muda wa kusoma tofauti na ule wa kufanya mazoezi, ingawa itachukua muda kabla ya uwanja wa Afraha kukarabatiwa ili urudie hali ya kawaida.

“Huenda talanta nyingi zikapotea kwa sababu wachezaji wataagana na michezo, kwa sababu ya ukosefu wa uga wa kufanyia mazoezi.

Changamoto za kutumia mtandao wa kijamii

Kulingana na Wyne anasema sio kila mara mzazi ataweka hela katika simu ili aweze kufuatilia mpangilio wa ratiba ya kufanyia mazoezi kupitia mtandao.

Pili anaungama kuwa sio wachezaji wote ambao wanaweza kutumia mtandao wa kijamii kufanya mazoezi kwa sababu wengi wao wanatokea katika jamii maskini mitaani.

Kulingana na mkufunzi Mildred Ayanda anasema alikusudia kutumia mtandao wa kijamii ili kuwaleta pamoja wachezaji wake ili kuwaweka katika hali nzuri ya kiafya.

Ingawa sio rahisi kuwaunganisha wote wachache ambao wanapata msaada wa wazazi wao wanaweza kujiendleza ili kutumia wakati wao vyema katika kipindi hiki cha msimu mrefu.

Aidha mtandao wa kijamii umekuwa ukiadhiri mawazo ya wachezaji maana baadhi yao wamevunjika moyo kila wanapoona uwanja wa Afraha ukitumika kama soko kwa wafanyibiashara.

Kufikia sasa ligi ya Sub Branch ya divisheni ya pili FKF, ina jumla ya timu 42 ambapo ambapo kila timu inatakiwa kucheza jumla ya mechi 38.

Mkufunzi mzoefu Dickson Gitari anahoji kuwa timu ya Nakuru Youth Sports Association inaweza kutoa timu ya KPL,kuwakilisha Nakuru siku za mbeleni endapo miundo misingi itakarabatiwa.

Kulingana na Gitari anasema kuwa kutokana na janga la Covid-19, kufikia sasa timu nyingi zmecheza baina ya mechi 3-7 tu

“Ndiposa haitoshi kwa FKF kutoa mshind moja kwa moja, na janga hili limeadhiri pia timu zawatoto ambao wanalenga kupanda daraja katika uchezaji wa mpira,”aliongezea.

Isitoshe licha ya changamoto nyingi muungano wa Nakuru Mothers and Dads umeamua kuwekeza katika talanta za watoto mjini Nakuru ili kuwapatia wachezaji wenye vipaji fursa ya kunadi vipawa vyao.

Mojawapo ni kikosi cha Nakuru Youth ambacho kipo katika mazungumzo ya uhusiano mwema ili kuboresha hali ya soka nchini siku za baade ambayo inatishiwa kudorora kutokana na janga la Covid 19.

You can share this post!

AKILIMALI: Bayogesi inavyopunguzia wakulima gharama

Biashara ya vinyago inalipa

adminleo