• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
TENISI: Naomi Osaka aondolewa mapema kwenye Olimpiki 2020

TENISI: Naomi Osaka aondolewa mapema kwenye Olimpiki 2020

Na MASHIRIKA

MWANATENISI Naomi Osaka, 23, ameaga mapema mashindano ya Olimpiki baada ya kubanduliwa na Marketa Vondrousova wa Jamhuri Czech.

Osaka ambaye ni raia wa Japan alikuwa akipigiwa upatu wa kutwaa nishani ya dhahabu kwenye tenisi ya mchezaji mmoja kila upande katika ardhi yao ya nyumbani.

Hata hivyo, mshindi huyo mara nne wa Grand Slam alipokezwa kichapo cha 6-1, 6-4 na Vondrousova ambaye kwa sasa anaorodheshwa katika nafasi ya 42 duniani.

“Presha ilikuwa tele kwangu kufanya vyema katika mashindano haya ambayo kwa kweli sikuwa na tajriba yoyote ya kuyashiriki. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kunogesha Olimpiki, presha ilitarajiwa kuwa kubwa,” akasema Osaka ambaye kwa sasa anashikilia nafasi ya pili duniani.

Osaka ambaye ni bingwa wa US Open na Australia Open, alikuwa ameshinda michuano 25 kati ya 26 kabla ya kushuka ulingoni kwa ajili ya Olimpiki za Tokyo, Japan.

Mashindano hayo yalikuwa ya kwanza kwa Osaka kushiriki tangu ajiondoe kwenye kipute cha French Open mnamo Juni 2021 baada ya kulalamikia msongo wa mawazo tangu aibuke mshindi wa Grand Slam mnamo 2018.

Baada ya kushinda raundi mbili za kwanza kirahisi, Osaka alitarajiwa kuendeleza ubabe huo dhidi ya Vondrousova ambaye ni mshindi wa zamani wa taji la French Open.

Hata hivyo, alifanya makosa 32 dhidi ya nyota huyo raia wa Jamhuri ya Czech mwenye umri wa miaka 22.

Kudenguliwa kwa Osaka kunajiri siku moja baada ya kubanduliwa kwa Ashleigh Barty wa Australia ambaye kwa sasa anashikilia nafasi ya kwanza kwenye orodha ya Shirikisho la Tenisi ya Wanawake Duniani.

Vondrousova sasa atacheza dhidi ya Paula Badosa wa Uhispania au Nadia Podoroska wa Argentina kwenye hatua ya robo-fainali.

Elina Svitolina wa Ukraine ndiye mchezaji anayeorodheshwa katika nafasi ya juu zaidi duniani (nambari tisa) ambaye sasa amesalia kwenye kipute cha Olimpiki. Alijituma maradufu kabla ya kumbandua Maria Sakkari wa Ugiriki kwa 5-7, 6-3, 6-4.

Belinda Bencic wa Uswisi alimpiku bingwa wa French Open, Barbora Krejcikova wa Jamhuri ya Czech kwa 1-6, 6-2, 6-3 huku Garbine Muguruza akimbwaga Alison van Uytvanck kwa 6-4, 6-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chipukizi wa Uingereza U-21 wapata kocha mpya

Malkia Strikers warejea uwanjani kesho dhidi ya Serbia