• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Tim Wanyonyi hatimaye atangaza kuunga mkono Igathe kwa kiti cha ugavana Nairobi

Tim Wanyonyi hatimaye atangaza kuunga mkono Igathe kwa kiti cha ugavana Nairobi

NA CHARLES WASONGA

HATIMAYE Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi ametangaza hadharani kuwa atamuunga mkono Polycarp Igathe ambaye wiki jana alitawazwa kuwa mgombeaji wa ugavana wa Nairobi chini ya mwavuli wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Bw Wanyonyi alikuwa katika kinyang’anyiro hicho hadi Ijumaa wiki jana, aliposhauriwa kujiondoa ili ampishe Bw Igathe ambaye aliteuliwa na Jubilee kuwania ugavana wa Nairobi.

Hii ni baada ya muungano huo kukubaliana kuwasilisha mgombeaji mmoja kwa kiti hicho ambaye atapambana na mwaniaji wa muungano wa Kenya Kwanza Seneta Johnson Sakaja.

Kwenye tangazo ambalo lilitolewa na mgombea urais wa Azimio Raila Odinga, Bw Wanyonyi alishauriwa kutetea kiti chake cha Westlands katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Kibwezi Profesa Philip Kaloki aliteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Igathe ambaye hadi kuteuliwa kwake alihudumu kama Meneja wa Masuala ya Kibiashara katika Benki ya Equity.

Kwenye picha zilizochapishwa katika akaunti ya Twitter ya Wanyonyi, mbunge huyo anaonekana akibadilishana kofia na Bw Igathe, ishara ya kumuunga mkono. Wawili hao wanaonekana wakitaniana kwa furaha.

“Nimemtembelea mgombeaji ugavana wa Azimio la Umoja-One Kenya Bw Polycarp Igathe. Nitamuunga mkono. Asante,” Bw Wanyonyi akasema.

Bw Igathe alikuwa ameandamana na Mbunge wa Kamukunji Yusuf Hassan, Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kaunti ya Nairobi Peter Imwatok na shabiki mkuu wa kandanda Tom Alila.

Bw Wanyonyi alitoa tangazo hilo siku moja baada ya Bw Sakaja ambaye ni mgombea ugavana wa Nairobi kwa tiketi ya Kenya Kwanza, kutangaza kuwa atafanya kazi kwa ukaribu na Bw Wanyonyi kwa lengo la kutwaa kiti cha ugavana wa Nairobi.

Bw Sakaja alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kupokea cheti cha kuwania ugavana wa Nairobi kwa tiketi ya chama cha UDA, katika makao makuu ya chama hicho, Nairobi.

“Tulikubaliana kwamba tutafanya kazi pamoja kwa sababu kwa ajili ya kufaulisha maono yetu ya kuendeleza jiji la Nairobi. Maelezo kamili yatatolewa baadaye lakini makundi yetu yanafanya kazi pamoja,” Bw Sakaja akasema.

Kumekuwa na uvumi kwamba Wanyonyi na Sakaja walikuwa wakipanga kufanya kazi pamoja baada ya wawili hao kuonekana pamoja Ijumaa muda mfupi baada ya Azimio kumteua Bw Igathe kuwa mgombeaji wa ugavana wa Nairobi

Lakini siku chache baadaye Bw Wanyonyi alitangaza kuwa atashindania kiti cha ubunge cha Westlands kwa muhula wa tatu.

“Azma yangu kama kiongozi huwa ni kuwahudumia watu. Natumai kuwahudumia wakazi wa Westlands kwa muhula wa tatu,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa walia bei ya juu ya...

LEONARD ONYANGO: Serikali iwekeze zaidi katika miradi ya...

T L