• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Tottenham Hotspur waajiri Antonio Conte kuwa mrithi wa kocha Nuno Espirito

Tottenham Hotspur waajiri Antonio Conte kuwa mrithi wa kocha Nuno Espirito

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wamemwajiri kocha wa zamani wa Chelsea na Inter Milan, Antonio Conte, 52, kwa mkataba wa miaka miwili.

Kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kimemteua Conte kuwa mrithi wa Nuno Espirito Santo aliyepigwa kalamu mnamo Novemba 1, 2021 baada ya kusimamia mechi 17 pekee.

Chini ya Nuno aliyehudumu kambini mwa Spurs kwa miezi minne pekee, kikosi hicho kilisajili msururu wa matokeo duni yanayowaweka katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

Kwa mujibu wa Spurs, bodi yao ya usimamizi itakuwa radhi kurefusha mkataba wa Conte kutegemea matokeo yatakayosajiliwa na mkufunzi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia.

“Nafurahia sana kurejea uwanjani kuwa kocha, mara hii nikidhibiti tena mikoba ya kikosi cha EPL kinachotawaliwa na azma ya kuwa miongoni mwa wagombezi halisi wa mataji ya haiba kubwa,” akasema Conte.

Conte ambaye ni raia wa Italia, anarejea London baada ya kushindia Chelsea taji la EPL katika msimu wake wa kwanza ugani Stamford Bridge (2016-17) na Kombe la FA katika msimu wake wa pili kabla ya kupigwa kalamu mnamo 2018.

Mkufunzi aliongoza Inter Milan baadaye kunyanyua taji la kwanza la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11 mnamo 2020-21 kabla ya kujiuzulu Mei 2021.

Conte alikuwa amehudumu kambini mwa Inter Milan kwa miaka miwili kikosi hicho kilipoagana naye akisalia na mwaka mmoja zaidi kwenye kandarasi yake.

Kabla ya Spurs kumwajiri Nuno, Conte alikuwa miongoni mwa wakufunzi wa kwanza kuzungumziwa na kikosi hicho kuhusu uwezekano wa kumwajiri kuwa mrithi wa Jose Mourinho aliyetimuliwa kwa sababu ya matokeo duni.

Mechi ya kwanza ya Conte kambini mwa Spurs ni gozi la Europa League litakalowakutanisha na Vitesse Arnhem ya Uholanzi mnamo Novemba 4, 2021 kabla ya kuendea Everton uwanjani Goodison Park siku nne baadaye.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wamalwa atoa hakikisho la upatikanaji wa haki kwa familia...

Aguero kutochezeshwa na Barcelona kwa miezi mitatu ijayo...

T L