• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Tshisekedi asutwa kuingiza wageni mgogoro wa DRC

Tshisekedi asutwa kuingiza wageni mgogoro wa DRC

Na MASHIRIKA

KINSHASA, DRC

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi, anashutumiwa kwa kuhusisha mataifa mengine katika kutatua mgogoro wake wa kiusalama.

Viongozi mbalimbali katika nchi hiyo wanadai kuwa Rais huyo anafaa kutatua migogoro kama hiyo kivyake bila kuhusisha mataifa mengine.

Wakiongozwa na Dkt Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2018, viongozi hao walimkosoa Rais huyo kwa kushindwa kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa.

Viongozi hao wanasema kuwa badala ya kiongozi huyo kuipa nchi jeshi madhubuti, serikali ya Tshisekedi imeamua kuuweka usalama wa taifa kwenye mikono ya mataifa ya kigeni.

Rwanda na Uganda ambazo ni nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa zikishutumiwa kwa muda mrefu kwa kuchochea mgogoro mashariki mwa Congo.

Nchi hiyo inapambana na kundi lenye silaha linaloitwa M23, ambalo limeteka maeneo mengi katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Huku majeshi ya DRC yakihangaika, Tshisekedi ametoa wito kwa jumuiya ya mataifa saba, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kupeleka wanajeshi ili kusaidia kupambana na kundi hilo.

DRC hasa inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 madai ambayo Rwanda imekuwa ikipinga ingawa madai hayo yaliungwa mkono katika ripoti mpya ya wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa.

“Badala ya kutatua matatizo yetu kivyetu, serikali inatilia maanani maoni ya mataifa mengine. Hii inafanya nchi kuyumba na kukosa mwelekeo thabiti,” walisema viongozi hao watatu kwenye mkutano wao.

Kikosi cha EAC kiko chini ya amri ya Kenya na wanajeshi wa Kenya walishatumwa katika nchi hiyo kusaidia kupambana na kundi hilo hatari.

Kundi la M23, chini ya shinikizo la jumuiya ya kimataifa, lilikabidhi mji wa kimkakati wa Kibumba kwa jeshi la EAC.

Malalamishi hayo yanakuja siku chache baada ya kundi la waasi la M23 kuonyesha dalili ya kusitasita kuhusu ikiwa litashiriki kwenye juhudi za kurejesha DRC katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hili ni licha ya viongozi kadhaa wa nchi shirika za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusema kuwa waasi hao wako huru kushiriki katika mazungumzo hayo.

Tshisekedi, mwanasiasa mkongwe wa upinzani, alichaguliwa kuwa rais Desemba 2018. Alimrithi Joseph Kabila, ambaye alitawala nchi hiyo tangu 2001.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Mwalimu avuna faida za kuzamia kilimo

Dkt Vincent Gaitho wa MKU ashinda tuzo kwa kazi nzuri

T L