• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Tundu Lissu apigwa marufuku kushiriki kampeni uchaguzi ukinukia

Tundu Lissu apigwa marufuku kushiriki kampeni uchaguzi ukinukia

Na THE CITIZEN

KAMATI ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC), imempiga Tundu Lissu marufuku ya kushiriki kampeni kwa siku saba.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo, Lissu ambaye ni mwaniaji wa urais kwa tiketi ya chama cha Chadema, alikiuka baadhi ya kanuni za uchaguzi katika mikutano ya kisiasa aliyoiandaa na kuhudhuria wakati wa kampeni zake.

Malalamishi dhidi ya Lissu yaliwasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi na vyama viwili vya kisiasa nchini Tanzania – Chama cha Mapinduzi (CCM) na NRA.

Katika taarifa yake, Katibu wa Kamati ya Maadili ya NEC, Emmanuel Kavishe alisema kwamba mnamo Oktoba 2, 2020 malalamishi dhidi ya Lissu aliyetoa kauli tata dhidi ya wapinzani wake yaliwasilishwa afisini mwake.

Kwa mujibu wa Kamati, Lissu alidai kwamba Rais John Pombe Magufuli alikuwa ameandaa mkutano na maafisa wa uchaguzi kote nchini kwa nia ya kuvuruga mchakato mzima wa uchaguzi.

Aidha, Lissu alitoa madai yaliyolenga kudunisha wawaniaji wengine wa urais kinyume na kanuni za maadili.

Kavishe alisema Lissu alishindwa kutoa ithibati kwa madai hayo aliyoyatoa katika mkutano wa kisiasa alioufanya mjini Mara.

“Kamati ya Maadili ya NEC imeridhishwa na habari za ukiukaji wa maadili dhidi ya Tundu Lissu kwa mujibu wa Kifungu cha 39 katika Katiba ya 1977 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

“Lissu, mwaniaji wa urais kupitia chama cha Chadema, alitoa kauli za utata zilizolalamikiwa na wagombezi wenzake kupitia NEC na ameshindwa kuyathibitisha,” akasema.

Majuzi, NEC ilimpa Lissu barua ya kumtaka kuonyesha ithibati ya madai aliyokuwa akitoa dhidi ya washindani wake kwenye uchaguzi ujao. Hata hivyo, katika kampeni zake mnamo Alhamisi ya Oktoba 1, Inspekta Mkuu wa Polisi Simon Siro alimtaka Lissu kujiwasilisha kwa Kituo cha Polisi cha Moshi.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chipu sokoni kutafuta kocha Murunga, Ocholla na Habimana...

Olunga apata mabao mawili Kashiwa ikilima Yokohama