• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:10 PM
TUZO KUU YANUKIA: Gwiji Cheruiyot, Kipchoge katika orodha ya IAAF

TUZO KUU YANUKIA: Gwiji Cheruiyot, Kipchoge katika orodha ya IAAF

Na CHRIS ADUNGO

ELIUD Kipchoge atakuwa miongoni mwa watimkaji watakaowania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka Duniani kwa upande wa wanaume katika tuzo zitakazotolewa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) jijini Monaco, Ufaransa mnamo Novemba 23.

Kipchoge aliweka historia mnamo Oktoba 12 kwa kuwa binadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili aliposhiriki kivumbi cha INEOS 1:59 Challenge jijini Vienna, Austria.

Bingwa huyo wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon alikamilisha kivumbi cha INEOS 1:59 Challenge baada ya muda wa saa 1:59:40.2.

Mkenya mwingine aliyeteuliwa kuwania ufalme wa taji hilo ni Timothy Cheruiyot aliyetwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa majuzi jijini Doha, Qatar.

Cheruiyot aliyetawazwa bingwa wa Diamond League mnamo 2017, 2018 na 2019, amewahi pia kunyakua nishani ya fedha katika mbio za mita 1,500 wakati wa Riadha za Dunia zilipoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.

“IAAF imetoa orodha rasmi ya watimkaji 11 watakaowania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanaume. Uteuzi wao umechangiwa na ubora wa matokeo yao katika Riadha za Dunia, Diamond League na mbio za marathon na nyika,” ikasema sehemu ya taarifa ya IAAF iliyosisitiza kwamba makala ya Riadha za Dunia yaliyoandaliwa Qatar mwaka huu ndiyo bora zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mapambano hayo.

Wanariadha wengine watakaopania kuwapiku Kipchoge na Cheruiyot ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 800, Donavan Brazier wa Amerika na mwenzake Christian Coleman ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 100 na Joshua Cheptegei wa Uganda ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za nyika na mita 10,000.

Wengine ni Steven Gardiner wa Bahrain (mbio za mita 400), Sam Kendricks wa Amerika (kuruka kwa pondo), Noah Lyles wa Amerika (mbio za mita 200), Daniel Stahl wa Uswidi (urushaji kisahani) na Karsten Warholm wa Norway ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 400 kuruka viunzi.

Orodha ya wawaniaji wa kike ilitarajiwa kutolewa baadaye jana.

Mafanikio ya Kipchoge, aliyevunja rekodi ya dunia katika mbio za marathon mwaka jana, ni kati ya matukio yaliyomfanya kutawazwa Mwanariadha Bora wa Mwaka wa 2018 kwa upande wa wanaume katika tuzo za IAAF zilizotolewa nchini Ufaransa.

Caterina Ibarguen wa Colombia ambaye ni bingwa wa dunia katika fani ya kuruka mbali ndiye aliyetia kapuni taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake baada ya kumpiga kumbo Beatrice Chepkoech.

Washindani wakubwa zaidi wa Kipchoge katika tuzo za 2018 walikuwa bingwa wa decathlon, Kevin Mayer kutoka Ufaransa na mtimkaji matata wa Amerika, Coleman.

Mnamo 2018, Coleman, 22, alivunja rekodi ya mbio za ndani ya kumbi katika mita 60 huku akitawala pia mbio za mita 100 katika Diamond League.

Mayer, 27, aliibuka mshindi wa heptathlon na kuivunja rekodi ya dunia katika decathlon kwa kuzoa jumla ya pointi 9,126 zilizoboresha rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na raia wa Amerika Ashton Eaton.

Chepkoech aliyehifadhi ubingwa wa dunia jijini Doha mwaka huu, aliboresha rekodi ya dunia katika mbio za mita 3000 kuruka maji na viunzi kwa sekunde nane mnamo 2018 kwa kukamilisha Herculis Diamond League kwa muda wa dakika 8:44.32.

Kwa sasa, anashikilia rekodi ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji ambayo aliweka mjini Fontvieille, Monaco akivunja rekodi ya Mbahrain Ruth Jebet mnamo Julai 2018.

Hadi kutuzwa kwa Kipchoge mnamo 2018, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 David Rudisha alikuwa ndiye Mkenya wa pekee aliyewahi kuibuka Mwanariadha Bora duniani aliponyakua taji la mwaka 2010 tangu hafla ya kutuza wanariadha bora ianzishwe mnamo 1988.

Washiriki wa mwaka huu watapigiwa kura na umma kupitia mitandao ya kijamii ya IAAF.

Baraza la IAAF na familia ya IAAF watatumia baruapepe.

Asilimia 50 ya kura za Baraza la IAAF na asilimia 25 ya kura za familia ya IAAF na asilimia 25 zilizopigwa na umma zitatumika kuamua washindi wa taji la mwanariadha bora wa mwaka kwa upande wa wanaume na wanawake.

You can share this post!

Ronaldo awika huku Ureno ikiteswa mechi ya kusaka tiketi...

Umuhimu wa shukurani

adminleo