• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
UANDISHI: Mathias Momanyi ni mwandishi mahiri wa vitabu vya Kiswahili

UANDISHI: Mathias Momanyi ni mwandishi mahiri wa vitabu vya Kiswahili

Na PETER CHANGTOEK

KWA wale waliokuwa wakiyapenda makala yake ya ‘Shule ya Shangaa’ yaliyokuwa yakichapishwa katika gazeti la Taifa Leo, ni vigumu sana kwao kusahau vitushi pamoja na sarakasi zilizokuwa zikifanyika shuleni huko.

Bw Mathias Momanyi ‘Mzee Mzima’ aliitumia jazanda katika makala hayo na kwa hakika wasomaji walifaa kuwa na hekima ili kuuelewa ujumbe ambao mwandishi huyo mashuhuri alikuwa akinuia kuuwasilisha kwao.

Kwa mujibu wa mwandishi huyo, Shangaa haikuwa shule, bali ni jazanda tu aliyoitumia kuisawiri nchi ya Kenya, pamoja na raia, na jinsi rasilimali ya nchi itumiwavyo ndivyo sivyo na viongozi.

Mbali na kuwa mwandishi wa vitabu na mtangazaji katika Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), Mathias Momanyi ana kipaji kingine ambacho wengi huenda hawakijui. Yeye amezitunga na kuzirekodi nyimbo kadhaa ambazo wengi huita ‘muziki wa kufokafoka’ au ‘rap music’.

“Jina langu la kisanii ni ‘Kamusi Inayotembea’. Nina nyimbo nne; ‘Wimbi Takatifu’, ‘Mama’, ‘Usidunde’ na ‘Niporadi’. ‘Wimbi Takatifu’ ni wimbo uchezwao sana katika vyombo vya habari, na niliutunga baada ya binamu yangu, Walter Mong’are Nyambane kuurekodi wake, ‘Sweet Banana,’’ anafichua msanii huyo ambaye pia ni mwandishi wa vitabu na mtangazaji.

SWALI: Tupe historia kukuhusu. Wewe ni nani, na ulizaliwa wapi?

JIBU: Majina yangu kamili ni Mathias Momanyi, mzaliwa wa maeneo ya Ikuruma, katika vitongoji na milima ya Kisii. Nililelewa katika mazingira tofauti tofauti, na hii ni kutokana na chimbuko na fasili ya wazazi wangu. Sijatimiza miaka ya ukongwe zaidi kuitwa mzee, japo natumia lakabu ya ‘Mzee Mzima’. Nina umri wa miaka 38. Babangu anaitwa Profesa Omar Odari Kienga, japo anajulikana kwa jina jingine kama Zephaniah Nyarunda, na mamangu anaitwa Raeli Nyatundo ambaye asili yake ni eneo la Mbezi, Tanzania. Mie ni mzawa wa pili katika familia yetu. Babangu hukipenda Kiswahili na alikuwa msimazi katika kitengo cha elimu Pwani, lakini amestaafu na mamangu ni mwalimu na mwimbaji.

Familia yetu ni kubwa sana maadamu babu yetu alikuwa na wake zaidi ya kumi na familia yetu ina wanahabari wengi kama vile Walter Mong’are Nyambane (binamu), ndugu yangu Vincent Momanyi (Radio One, Tanzania). Dadangu pia ni mtangazaji katika Sayari FM.

SWALI: Tupe maelezo kuhusu elimu yako. Ulisomea wapi?

JIBU: Nilisomea Shule ya Feza jijini Dar es Salaam, Tanzania, Shule ya Msingi ya Mutundo, Kisii, kisha nikasomea Shule ya Upili ya Nyambaria, huko Kisii. Nilisomea pia shule za upili za Bushangala na St. Peter’s Mumias. Baada ya kukamilisha masomo yangu ya shule ya upili, nikajiunga na Chuo cha Ualimu cha Asumbi na Kagumo T.T.C. Kwa hivyo, nina taaluma mbili za ualimu. Kisha nikajiunga na Chuo Kikuu cha Moi, nilikosomea shahada ya Sayansi ya Mawasiliano. Nilisoma pamoja na Ali Manzu na Mohamed Ali katika Chuo Kikuu cha Moi, bewa la Nairobi.

SWALI: Kabla hujawa mtangazaji, uliwahi kuifanya kazi ya ualimu?

JIBU: Nilifanya kazi ya ualimu katika Shule za Makini, zilizoko katika Barabara ya Ngong. Nilikuwa nikifunza pamoja na Ustadh Wallah Bin Wallah na Jack Oyoo Sylvester. Pia, nilifundisha katika shule ya Consolata, Westlands, chini ya padri mmoja aitwaye Caroli Ouma Ogeda ambaye ni mpenzi wa Kiswahili sana. Nilikuwa nikifunza katika Shule za Makini, huku nikiendelea kusomea taaluma ya uanahabari, lakini hakuna yeyote aliyekuwa akijua hivyo. Nilifunza katika Makini kutoka mwaka 2005 hadi 2012.

SWALI: Ulikuwa shabiki sugu wa kipindi ‘Kamusi ya Changamka’ katika Nation FM ambacho kwa wakati huu hupeperushwa hewani kupitia QFM na QTV kila Jumamosi kuanzia saa moja hadi saa tano za asubuhi. Je, kipindi hicho kilichangia ubora wako wa lugha ya Kiswahili?

JIBU: Ndiyo. Kwa hakika tulikuzana katika lugha ya Kiswahili. Nakumbuka enzi hizo tukichangia na wapenzi wa Kiswahili kama vile; Ustadh Wallah Bin Wallah, Anduvate K.M, Swila Mchiriza Sumu (Salim Bakari), Muriuki Gikunju, Samuel Muriuki, Athur Andambi ambaye kwa sasa yupo ughaibuni na wengine.

SWALI: Ulijiunga na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) lini?

JIBU: Mwaka 2014, KBC ilitangaza nafasi ya kazi, nikatuma maombi, kisha nikaitwa kwa mahojiano. Niliajiriwa kuwa mtayarishi mwandamizi, yaani ‘Senior Producer -SS1’. Kwa sasa, ninasimamia mtandao wa Kiswaili wa KBC Radio Taifa, nikishirikiana na ndugu Jared Ombui. Pia, hukipeperusha kipindi ‘Ramani ya Kiswahili’ kila Jumamosi asubuhi hadi saa tano. Fauka ya hayo, mie huendesha kipindi ‘Vuvuzela’ kila Jumapili kuanzia saa mbili hadi saa sita za usiku.

SWALI: Mbali na amali ya utangazaji, wewe pia ni mwandishi wa vitabu vya Kiswahili. Kufikia sasa, umeviandika vitabu vingapi?

JIBU: Nimeviandika vitabu takribani 15. Vile rasmi ambavyo viko sokoni ni 10.

SWALI: Baadhi yavyo ni vipi?

JIBU: ‘Hazina na Abdul’ kilichochapishwa na EAEP (2011), ‘Lisani za Lusufu’ ambacho kilichapishwa na Faulu Publishers (2006). Hiki ni kitabu cha msamiati, ambacho niliamua kukiandika baada ya wapenzi wengi wa Kiswahili na baadhi ya walimu kunipa jina ‘Kamusi Inayotembea’. Ni kitabu kilichopata ukinzani mkubwa sana kutoka kwa baadhi ya wanahabari, hususan kutokana na msamiati ‘Mwanasheria Mkuu’ (Attorney General), nilioupachika kitabuni kinyume cha matarajio ya wengi waliokuwa wamezoea kuutumia msamiati ‘mkuu wa sheria’. Lakini wengi wameafikiana nami! Pia kuna hadithi ‘Shujaa Mateso’ (EAEP, 2013), ‘Nyota ya Ufasaha’ ambacho ni kitabu cha insha kilichochapishwa na Faulu Publishers mwaka 2003. ‘Taabu za Tabu’ (EAEP, 2014), ‘Kurunzi ya Marejeleo Halahala ya Kiswahili’, kilichochapishwa na Spotlight Publishers wakati huo, Target Publishers. Pia, nilishirikiana na Yahya Mutuku kuandika ‘Kilele cha Insha 1-3’, ‘Kilele cha Insha 4 na 5’ na ‘Kilele cha Insha 6-8’. Vile ambavyo havijachapishwa ni ‘Ngoma’ (tamthilia) na ‘Mimba ya Mwendawazimu’ (riwaya).

SWALI: Je, ni kina nani waliokutia motisha hadi ukaamua kuwa mtangazaji na mwandishi wa vitabu?

JIBU: Namshukuru sana Bw Simon Sossion (mkurugenzi wa Spotlight Publishers) kwa kuwa mlezi wangu wa lugha ya Kiswahili. Alikiona kipawa changu alipokuwa mkurugenzi na mhariri katika shirika la Longhorn. Sitamsahau Ustadh Wallah Bin Wallah ambaye tulisemezana na nikazishika kauli zake. Wengine walionitia motisha ni Mohamed Seif Khatib, Profesa Adam Shafi, Profesa Said Ahmed Mohamed, Al Ustadh Ngatuma (Zanzibar), Ali Hassan Kauleni (Nuru ya Lugha, Radio Maisha), Nuhu Zuberi Bakari (Kamusi ya Changamka, QFM), Fred Obachi Machoka, Waweru Mburu, Esther Macharia, Fred Afune, Waithaka Waihenya (mwandishi na mkurugenzi, KBC), James Mwaura, Martin Nyongesa King’asia, Nicholas Muema, Maxim Musyoki, Hezekiel Gikambi miongoni mwa wengine.

SWALI: Ni changamoto zipi ambazo umewahi kuzipitia katika utangazaji?

JIBU: Changamoto kuu ni pingamizi na hata ukinzani kutoka kwa wale wasiokipenda Kiswahili. Ni muhali kwa wengine kukubali kukosolewa wanapokosea. Lakini sikati tamaa kwa hilo! Pia, unaweza kumwalika mtu aje studioni kisha baadaye asije kutokana na sababu fulani, ilhali ulikuwa umepachika habari katika mitandao ya jamii kuwa utakuwa naye studioni!

SWALI: Uraibu wako ni nini?

JIBU: Uraibu wangu mwingi ni kusoma vitabu. Mende wakishiba kwangu, hushiba vitabu! Na mapenzi yangu kwa vitabu yamenifanya kutembelea nchi nyingi sana na kukutana na marafiki mbalimbali.

SWALI: Je, umeoa?

JIBU: Nina mke (Oliphah Binti Khamis) na watoto wawili; Neema Salama na Zachariah Nyatundo.

SWALI: Ni ushauri gani unaowapa vijana ambao wananuia kuwa watangazaji au waandishi wa vitabu?

JIBU: Watimize ndoto zao kwa kunoa makali yao kwa maombi. Waweke imani zao kwa Mungu.

SWALI: Mipango yako ya siku za usoni ni ipi?

JIBU: Nataka kuwekeza zaidi kuliko nilivyowekeza sasa hivi. Pia nina mipango ya kuliasisi shirika ambalo litashughulikia vijana kutoka katika vitongoji duni, hasa wale ambao vipaji vyao havijagunduliwa ili wafike huku tuliko sisi.

 

You can share this post!

Muuzaji chang’aa aliyewapiga machifu wanne aachiliwa kwa...

MATUKIO YA 2019: Mafuriko yalivyotatiza wakazi Thika

adminleo