• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Omanyala kutia mfukoni Sh850,000 licha ya kushika nafasi ya saba mbio za Budapest

Omanyala kutia mfukoni Sh850,000 licha ya kushika nafasi ya saba mbio za Budapest

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Afrika na Jumuiya ya Madola mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala amelazimika kuridhika na Sh854,097 baada ya kumaliza nambari saba kati ya washiriki wanane kwenye Riadha za Dunia jijini Budapest, Hungary, Jumapili.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika aliyekuwa amepigiwa upatu kutwaa medali, alimaliza umbali huo kwa sekunde 10.07.

Majuma machache yaliyopita jagina wa Amerika Michael Johnson alikuwa amebashiriki kuwa umbo kubwa la afisa huyo wa polisi huenda likawa kizuizi kwake kupata medali na inaonekana ubashiri wake umetimia Agosti 20.

Baada ya kuponea tundu la sindano kukosa fainali akifuzu kama mmoja wa watimkaji waliomaliza nje ya nne-bora wakiwa na muda bora alipotimka sekunde 10.01, alionekana kujikokota katika fainali.

Mwamerika Noah Lyles (9.83), Letsile Tebogo kutoka Botswana (9.88) na Mwingereza Zharnel Hughes (9.88) wamezoa medali ya dhahabu, fedha na shaba, mtawalia.

Bingwa wa Kip Keino Classic Continental Tour na Monaco Diamond League, Omanyala alitangaza kuwa lengo lake kuu mwaka 2023 ni kutwaa taji la dunia pamoja na taji la jumla la Diamond League. Taji la dunia sasa limemponyoka na ataelekeza nguvu zake katika Diamond League.

  • Tags

You can share this post!

Barobaro anavyounda hela kama njugu kupitia uchakataji...

Magavana wageuka kuwa ‘miungu’ badala kuwa watumishi

T L