• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
UCHUKUZI: Anafanya kazi ya kubebea wakulima mazao yao

UCHUKUZI: Anafanya kazi ya kubebea wakulima mazao yao

Na SAMMY WAWERU

ALIPOHAMIA eneo la Thika miaka kadha iliyopita, alilenga kuimarisha maisha yake.

Eric Mutunga, 27, kutoka Masaku, Kaunti ya Machakos anasema kazi ya kwanza iliyomkaribisha ni utunzaji wa makazi ya kupangisha eneo la Ngoigwa, maarufu kama ‘keateka’.

Mchagua jembe si mkulima, barobaro huyo hakuwa na budi ila kuchapa kazi. Ikizingatiwa kuwa suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana limesalia kuwa ndugu nchini, Mutunga alifanya kazi kwa bidii.

“Sikujalishwa na kiwango cha mshahara niliopokea, kidogo kidogo hujaza kibaba,” anasema.

Kijana huyo alijikakamua na kuweka akiba, ambapo alinunua punda na kijigari chake – mkokoteni.

“Punda alinisaidia kuimarisha mapato yangu, ambapo nilimtumia kubebea watu mizigo,” anaeleza.

Alilenga wafanyabiashara hasa wenye maduka, wakulima na mikahawa ili kuisafirishia maji yanapoadimika.

Kulingana na Mutunga  gange hiyo ilinoga kiasi cha kumuwezesha kununua pikipiki. Hata hivyo, jitihada zake nusra zizimwe alipohusika katika ajali mbaya na punda wake.

“Nilivunjika mguu baada ya kuangushwa na punda nikiwa kwenye mkokoteni,” anasimulia mjasirimali huyo.

Mutunga anaiambia Taifa Leo kwamba alipopata nafuu aliingilia shughuli za uchukuzi na usafiri kutumia pikipiki.

Anasema aliendeleza ubebaji wa mizigo ya wafanyabiashara na wakulima.

“Huingia mashambani na kusafirishia wakulima na kina mama mboga mazao,” anadokeza.

Mengi ya mashamba hayaingiliki kwa magari kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Mutunga anasema wahudumu wa bodaboda ndio hutumika kusafirisha mazao.

Eneo la Ngoigwa ingawa limesheheni majumba ya kupangisha, kijana huyo anasema kuna wanaofanya shughuli za kilimo kama vile kukuza mboga, nyanya, vitunguu, karoti, pilipili mboga, na mimea mingineyo.

Kijana Eric Mutunga hufanya kazi ya ubebaji wa mazao ya kilimo na bidhaa za biashara. Picha/ Sammy Waweru

Malipo yanategemea maelewano, japo Mutunga anasema kila uchukuzi haupungui Sh300.

“Wafanyabiashara ni wamiliki wa maduka yanayouza bidhaa mbalimbali, na baadhi yao hunipa vibarua kuwabebea mizigo,” anasema.

Kando na kufanya shughuli za uchukuzi wa mizigo, barobaro huyo pia hujishughulisha na kazi ya uanabodaboda.

“Hubeba abiria majira ya jioni, kwa muda wa saa mbili pekee,” Mutunga ambaye ni baba wa mtoto mmoja anadokeza.

Baadhi ya vijana licha ya kuwa wamesoma, wameendelea kuwa mateka wa utafutaji wa ajira za ofisi na ambazo hazipatikani. Kila mwaka maelefu hufuzu kwa vyeti vya masomo kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu, na Mutunga anasema umewadia wakati vijana wapevuke na kujiajiri.

“Kazi za juakali zinalipa, wazitumie kujiimarisha kimaisha badala ya kutegemea ajira zisizopatikana,” anashauri.

Juakali inaorodheshwa katika sekta ya biashara ndogondogo na zile za wastani (SMEs), na ambazo zinakadiriwa kuwakilisha zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini, yaani inayoongoza katika ubunifu wa ajira.

Mhasibu na mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, Bw Michael Muriuki anasema suala la ukosefu wa kazi Kenya, hasa miongoni mwa vijana, litatatuliwa iwapo watakubali kuingilia shughuli za juakali.

“Juakali ina mianya mingi mno kujiajiri na hata kubuni nafasi kwa wengine,” anasema Bw Muriuki.

Kwa mfano, kujiri kwa bodaboda nchini kumebuni nafasi za kazi kwa mamekanika na wanaouza vipuri vya kukarabati pikipiki. Aidha, bodaboda ziliingia nchini chini ya utawala wa Rais wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

You can share this post!

Inspekta apatikana amefariki katika baa eneo la Bombolulu

Maseneta wamuunga Yatani kuzinyima fedha kaunti zenye...

adminleo