• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
UDIKTETA AFRIKA: Marais waliokatalia madarakani

UDIKTETA AFRIKA: Marais waliokatalia madarakani

Na PETER MBURU

WANANCHI wa Cameroon Jumapili Oktoba 7 watakuwa wakishiriki zoezi la kutimiza haki yao ya kidemokrasia, watakapomchagua rais mpya atakayewaongoza.

Hata hivyo, uwezekano mkubwa ni kuwa watazidi kuongozwa na rais ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 36 hadi sasa, Rais Paul Biya, ambaye ameweka mikakati kuhakikisha kuwa anaendelea kutawala taifa hilo.

Bw Biya mwenye umri wa miaka 85 ni mmoja wa viongozi wachache duniani na Afrika walioongpoza kwa vipindi virefu zaidi, katika awamu zao watoto wakizaliwa, kusoma, kuoa na hata kuzeeka wakapata wajukuu bado wakiwa madarakani.

Bara la Afrika limekuwa likikumbwa na tetesi za uongozi mbaya ambao umezuia maendeleo ya kiuchumi kutekelezwa tangu alipoondoka mkoloni, kati mwa karne ya 20.

Licha ya kubuniwa kwa Muungano wa Afrika (AU) ambao ulikuja na maelekezo mapya na ishara ya mabadiliko kwa bara hili, takriban miongo miwili tangu kuundwa kwa AU bado mataifa mengi ya Kiafrika yamezongwa na umasikini, kutokana na uongozi usio wa maadili wala kuheshimu demokrasia.

Tatizo kubwa limekuwa viongozi wa mataifa kukataa kung’atuka madarakani pale wanapoonja utamu wa uongozi, wengine wao wakiishia kubadilisha katiba za nchi zao ili kujiongezea muda wa uongozi, wazidi kuwa kileleni.

Baadhi ya Marais, waliopo hadi sasa, waliokufa ama walioondolewa kwa nguvu waliongoza kwa miongo, wakiishia kupotoka, kutojali haki za wananchi na kuzamisha mataifa yao.

Taifa Leo ilifanya utafiti kuhusu baadhi ya viongozi ambao waliwahi kuongoza ama hadi sasa bado wanaongoza kwa vipindi virefu zaidi, licha ya muda waliotarajiwa kuongoza kuisha.

1. Teodoro Obiang – Equitorial Guinea (Miaka 39)

Aliingia uongozini kupitia mapinduzi ya serikali mnamo 1979 na amekuwa akiongoza taifa leo hadi sasa. Rais huyo wa miaka 75 amekataa kung’atuka madarakani, sasa kitarajiwa kuendesha muhula huu hadi 2022, baada ya kushinda uchaguzi mnamo 2015.

2. Dennis Sassou Nguesso – Congo (Miaka 39)

Rais huyu (pichani) aliingizwa madarakani na jeshi mnamo 1979 na kuongoza Congo hadi 1997 ambapo aliondolewa kwa miaka mitano. Kutoka 1997, Bw Nguesso ameongoza nchi hiyo ambayo ina matatizo ya kiuchumi hadi leo.

3. Jose Eduardo Dos Santos – Angola (Miaka 38)

Bw Santos aliingia madarakani 1979 baada ya Rais wa kwanza wa taifa hilo kufa, miaka minne baada ya kujipatia uhuru. Hata hivyo, aliishia kuongoza kwa miaka 38. Hata hivyo, uongozi wake haukukashifiwa bali ulisifiwa kwa kuinua uchumi wa taifa hilo kutokana na kuboreshwa kwa sekta ya mafuta, rasilimali kuu ya taifa hilo.

4. Robert Mugabe – Zimbabwe (Miaka 37)

Rais Mugabe aliingia madarakani kama kiongozi wa kwanza wa Zimbawe mnamo 1980 na kuongoza kwa kifua hadi alipongólewa kwa nguvu mnamo 2017 akiwa na miaka 93, baada ya kuongoza kwa nguvu kwa miaka 37. Wakati wa kuondolewa kwake kwa nguvu, Bw Mugabe alikuwa amemteua mkewe kuwa makamu wake na alipanga kumfanya mridhi wake. Katika uongozi wake, taifa hilo limekumbwa na matatizo si haba ya kiuchumi na dhamani ya pesa zao kushuka kupita kiasi.

5. Paul Biya – Cameroon (Miaka 36)

Kiongozi huyo wa miaka 85 amekashifiwa kwa kuongoza nchi yake kienyeji, mara nyingi akiripotiwa kuwa nje ya taifa hilo. Uchaguzi nchini Cameroon utaandaliwa Oktoba 7 na Rais huyo atakuwa akigombea kiti hicho kwa mara ya saba, tangu alipoingia mamlakani mnamo 1982.

6. Yoweri Museveni – Uganda (Miaka 32)

Rais Museveni ambaye yuko madarakani hadi sasa ameongoza Uganda tangu 1986 alipochukua hatamu baada ya kuongoza mapinduzi. Alishinda uchaguzi wa mwisho mnamo 2016 baada ya kuongoza kwa miaka 30, japo chaguzi za nchi hiyo zimekuwa zikikumbwa na madai ya wizi wa kura. Utawala wake umekashifiwa vikali na kuhusishwa na uvunjaji wa haki za binadamu, majuzi zaidi kikiwa kisa cha mbunge na msanii Bobi Wine.

Marais wengine wa Kiafrika walioongoza kwa zaidi ya mihula miwili namna katiba za nchi nyingi hupendekeza ni Omar al Bashir wa Sudan ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 28, Idriss Deby wa Chad ambaye ameongoza kwa miaka 27, Isaias Afewerki wa Eritrea (Miaka 24) sawa na aliyekuwa rais wa Kenya Daniel arap Moi, Ismail Omar wa Djibouti (Miaka 18), Paul Kagame wa Rwanda (Miaka 17) na Joseph Kabila wa DRC (Miaka 16)

You can share this post!

Mtaala mpya waidhinishwa na waangalizi wa kimataifa

Ajabu ya gazeti la taifa kuchapisha habari kwa Kichina

adminleo