• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Ufaransa kileleni Viwango vya FIFA, Ujerumani yatupwa nambari 15

Ufaransa kileleni Viwango vya FIFA, Ujerumani yatupwa nambari 15

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wapya wa dunia Ufaransa wamerukia juu ya jedwali la viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) vilivyotangazwa Alhamisi na kushuhudia Ujerumani ikitupwa chini nafasi 14 hadi nambari 15.

Ufaransa ya kocha Didier Deschamps, ambayo ilipepeta Croatia 4-2 katika fainali jijini Moscow nchini Urusi mnamo Julai 15, imepaa nafasi sita. Ni mara yake ya kwanza kuongoza viwango hivi tangu mwaka 2001.

Inafuatiwa na majirani Ubelgiji, ambayo imeruka juu nafasi moja baada ya kukamilisha ziara ya Urusi katika nafasi ya tatu.

Brazil, ambayo ni nchi inayojivunia mataji mengi katika Kombe la Dunia (matano), imeteremka nafasi moja hadi nambari tatu.

Washindi wa nishani ya shaba katika Kombe la Dunia mwaka 1998 Croatia wameimarika nafasi 16 hadi nambari nne.

Mabingwa wa zamani wa dunia Uruguay na Uingereza wameruka juu nafasi tisa na sita hadi nambari tano na sita, mtawalia. Ureno na Uswizi zimeshuka chini nafasi tatu na mbili mtawalia hadi nambari saba na nane. Uhispania na Denmark zinashikilia nafasi ya tisa kwa pamoja baada ya kuruka juu nafasi moja na tatu, mtawalia.

Argentina iko chini nafasi sita hadi nambari 11. Chile, ambayo haikuwa nchini Urusi kwa Kombe la Dunia, imeshuka nafasi tatu hadi nambari 12 na inafuatiwa na Uswidi, ambayo imepaa nafasi 11.

Colombia imeimarika kutoka nafasi ya 16 hadi 14 nayo Ujerumani ikiporomoka kutoka nambari moja hadi 15 baada ya kubanduliwa nje ya Kombe la Dunia katika mechi za makundi.

Tunisia inasalia nambari moja barani Afrika, lakini 24 duniani baada ya kuteremka nafasi moja. Senegal ni ya pili Afrika. Imepaa nafasi tatu.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ghana, ambazo hazikufuzu kushiriki Kombe la Dunia, zinashikilia nafasi ya tatu na nne Afrika baada ya kuruka juu nafasi moja na nafasi mbili hadi 37 na 45 duniani, mtawalia. Morocco imeteremka nafasi tano hadi 46 duniani nayo Cameroon iko juu nafasi mbili hadi 47 duniani.

Nigeria imeteremka nafasi moja hadi 49 duniani baada ya kurukwa na Urusi, ambayo pia inashikilia nafasi ya 49.

Urusi iliingia Kombe la Dunia katika nafasi ya 70, lakini baada ya kutesa Saudi Arabia, Misri na Uhispania zilizoorodheshwa juu yao, sasa ndio timu iliyoimarika zaidi. Nayo Misri ni timu iliporomoka zaidi katika viwango hivi vya mataifa 206 baada ya kuteremka kutoka 45 hadi nafasi ya 65.

Eneo la Afrika Mashariki na Kati almaarufu Cecafa, linaongozwa na Uganda katika nafasi ya 82 duniani. Uganda haijabadilika kutoka nafasi hiyo sawa na Kenya, ambayo inashikilia nafasi ya pili Cecafa na 112 duniani.

Sudan (128 duniani), Rwanda (136), Tanzania (140), Burundi (148), Ethiopia (151), Sudan Kusini (156), Djibouti (197), Eritrea (206) na Somalia (206) zinafuatana kutoka nafasi ya tatu hadi 11 katika eneo la Cecafa.

You can share this post!

KCB yazoa faida ya Sh12 bilioni kwa miezi 6

Watano kati ya 7 watiwa nguvuni Homa Bay

adminleo