• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:41 PM
UFUGAJI: Afurahia ufugaji kuku wa mayai licha ya visiki vingi

UFUGAJI: Afurahia ufugaji kuku wa mayai licha ya visiki vingi

NA SAMMY WAWERU

PRISCA Njeri amekuwa katika biashara ya ufugaji wa kuku wa mayai kwa zaidi ya miaka saba.

Aliingilia ufugaji bila ufahamu kuhusu malezi ya kuku, akisema hakuona yeyote katika mazingira aliyoishi akifuga kuku kwa minajili ya biashara.

Aliojua, wakiwemo wazazi wake, walifuga kuku halisi wa kienyeji kupata mayai ya matumizi ya nyumbani na msimu wa Krismasi kuwageuza kitoweo.

Akiwa mke, ambaye jukumu lake kuu lilikuwa kutunza na kulea wanawe, Njeri alitafuta njia mbadala kujipa pato angalau kumpiga jeki mume wake.

Ufugaji ukawa ndio jawabu, na kwa mtaji wa Sh450,000 kiwango kikubwa kikiwa mkopo alianza mradi wa kuku.

“Nilianza na vifaranga 400,” mfugaji huyo afichua.

Hakujua kuku wa biashara kwa sababu ya kufugwa kwa idadi ya juu wanahitaji vizimba au makazi maalum, malezi na matunzo ya kipekee.

Kigezo kingine muhimu na nguzo kuu, ni unakotoa virafanga.

Wanapaswa kuwa wamepata chanjo dhidi ya magonjwa enezi ya ndege kama vile Newcastle, kukohoa, Gumboro na Marek’s.

“Safari yangu, nilikaribishwa kwa kupoteza vifaranga 250 kupitia Marek’s,” Njeri akumbuka, akikadiria hasara.

Anasema vizimba alivyotumia havikuambatana na idadi ya kuku alioanza nao, hivyo basi msongamano ukachochea masaibu yaliyompata.

Ni changamoto zilizomshurutisha kurejea ‘darasani’, kufanya utafiti wa ufugaji na malezi bora ya kuku.

Aidha, yanajumuisha kiwango cha boma, vifaranga waliopata chanjo, chakula, matibabu na maji.

“Mazingira pia ni muhimu, na kanuni za kuingia kwenye vizimba kuzuia maradhi enezi,” aelezea.

Amekumbatia mfumo huru, ambapo kuku wanalelewa eneo tambarare na kuruhusiwa kucheza – kuonyesha tabiahai zao.

“Kuku wanapaswa kuwa huru sakafuni, wacheze na kuzunguka kuboresha na kuimarisha viungo vya mwili, kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kimataifa kuhusu ufugaji wa wanyama na ndege,” ashauri Dkt Apollo Gichane, mtaalamu kutoka Kenchic.

Kenchic ni mojawapo ya kampuni tajika hapa nchini na Afrika Mashariki, inayotoa huduma za kuku hususan uanguaji vifaranga.

Njeri ambaye kwa sasa ameibuka kuwa mmoja wa wafugaji hodari, husambaziwa vifaranga na kampuni hiyo ya uzalishaji.

Akiwa mkazi wa Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, anaendeleza mradi wake kwenye kipande cha ardhi chenye kipimo cha futi 50 kwa 100, kwa sasa akiwa na kuku wapatao 1,600 wa mayai.

Ni kienyeji walioboreshwa, na anaambia Akilimali kwamba vizimba vyake vinaweza kusitiri hadi idadi jumla ya kuku 7, 500.

“Mfugaji akizingatia ubora wa makazi, vigezo faafu, malisho, matibabu, usafi na maji, biashara ya kuku ina faida,” Njeri asema.

Kreti ya mayai, bei ya rejareja haipungui Sh450 yai likichezea Sh15.

Ufugaji hata hivyo kipindi hiki si mteremko kwa sababu ya ongezeko la gharama ya chakula.

Dkt Gichane anasema kwa vifaranga waliochanjwa dhidi ya maradhi enezi, kiwango cha maafa huwa cha chini.

Wanapaswa kuchanjwa pindi wanapoanguliwa, aelezea, hivyo basi ni jambo muhimu mfugaji kufuatilia wanakotoka endapo hajiangulii.

Juni 7 kila mwaka ulimwengu huadhimisha Sikukuu ya Usalama wa Chakula Duniani, na Mkurugenzi Mkuu Kenchic, Jim Tozer anasisitiza kwamba mazao ya kuku yanapaswa kutiliwa maanani na mkazo.

Afisa huyo anahimiza haja ya wafugaji kuafikia vigezo na sheria za kuku kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kuhusu Afya ya Wanyama (OIE).

  • Tags

You can share this post!

Idadi ya waliokufa kwa bomu yafika 95

TUJIFUNZE UFUGAJI: Weka sheria kudhibiti wanaoingia kwenye...

T L