• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Ukaguzi: Kaunti ya Homabay imejaa wafanyakazi hewa, wengine ‘under-18’

Ukaguzi: Kaunti ya Homabay imejaa wafanyakazi hewa, wengine ‘under-18’

Na JESSE CHENGE
Uchunguzi umebaini kuwa Serikali ya Kaunti ya Homa Bay inaweza kuwa imepoteza Sh300 milioni zilizolipwa wafanyakazi hewa katika miaka iliyopita.
Ajira isiyo halali ya wafanyakazi iligunduliwa wakati wa ukaguzi wa sensa ya watu uliofanywa na wakaguzi wa Price Waterhouse Coopers mnamo Novemba 21 mwaka jana.
Ripoti iliyokabidhiwa Gavana Gladys Wanga Agosti 24, 2023 imebaini kuwa wafanyakazi hewa walijumuisha wale walio chini ya umri wa miaka 18 na wengine walioajiriwa wakiwa na miaka 16.
Ripoti hiyo, ambayo ilitolewa kwa umma na gavana kupitia mkutano na waandishi wa habari, ilifichua kuwa wafanyakazi hewa 1,786 walikuwa wakipokea mshahara kutoka kwenye mfumo wa Serikali ya Kaunti.
Ripoti ilionyesha kuwa watu 556 hawakuwasilisha barua za uteuzi wala nyaraka nyingine za ajira za kuaminika.
Wafanyakazi hewa hao walijumuisha watu 479 ambao wako kwenye mfumo wa malipo, lakini hawakuweza kufuatiliwa kwenye orodha za idara ya wafanyakazi.
Baadhi ya watu 287 hawakuonekana kabisa wakati wa zoezi la uchunguzi wa wafanyakazi.
Jumla ya watu 129 hawakuwa na faili yoyote katika usajili wa kaunti. Hawakuwasilisha nyaraka zozote zinazofaa wakati wa ukaguzi.
Kuna pia kundi lingine la watu 322 ambao hawakuwa na sifa za kitaaluma zinazofaa. Hii ni pamoja na wale ambao hawana leseni za kazi zilizotolewa na taasisi husika za kitaaluma wanazodai kuwa wanachama. Pia wanajumuisha watu ambao wana vyeti bandia vya Baraza la Mitihani la Kitaifa la Kenya (KNEC).
Kundi hili pia lilijumuisha watu ambao walidai kuwa walisoma katika vyuo na vyuo vikuu fulani lakini wakati vilipojaribu kuwasiliana nao, taasisi hizo zilikataa kuthibitisha ukweli wa vyeti vyao.
Watano kati yao walikamatwa huku wakitarajia kubuni na kuchapisha vyeti bandia katika mtandao huko Homa Bay.
Uchunguzi ulifichua kuwa wafanyakazi hao wamekuwa wakipokea mishahara inayofikia zaidi ya Sh300 milioni kila mwaka.
Wanga, ambaye aliandamana na Naibu wake Oyugi Magwanga, Katibu wa Kaunti Benard Muok na Mshirika wa PWC Simon Mutinda, alisema watafanyia kazi mapendekezo ya ripoti kwa kusafisha mfumo wa malipo.
Gavana alisema utekelezaji wa ripoti utasaidia kuokoa Serikali ya Kaunti zaidi ya Sh300 milioni kila mwaka.
“Malengo yetu ni kudhibiti matumizi ya mishahara na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa kushirikisha wataalamu waliohitimu,” alisema Wanga.
  • Tags

You can share this post!

Mbunge aliyeumizwa na wahuni afika DCI kwa kitimaguru

Wawili washtakiwa kudandia meli iliyobeba mibuyu kuelekea...

T L