• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Ukarimu wa Ruto wampa makanisa

Ukarimu wa Ruto wampa makanisa

NA BENSON MATHEKA

UKARIMU wa Naibu Rais William Ruto kwa viongozi wa makanisa umewafanya wengi wao kushindwa kujinasua kutoka kwake uchaguzi mkuu unapokaribia.

Kufikia Februari 2022, Dkt Ruto alikuwa akichangia makanisa kote nchini licha ya hatua yake kukosolewa na wapinzani wake akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga ambao wanaongoza muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Akitangaza kusitisha michango yake kwa makanisa kwa muda, Dkt Ruto alitaja sheria ya uchaguzi inayopiga marufuku michango wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

“Hatutafanya mchango wa ujenzi wa kanisa kwa sababu sheria ya uchaguzi hairuhusu. Lakini uchaguzi ukikamilika, ninaahidi kwamba tutarudi hapa na kuhakikisha ujenzi wa kanisa hili umekamilika,” Dkt Ruto alisema akiwa Emuhaya, Kaunti ya Vihiga mapema mwaka 2022.

Sheria ya Uchaguzi ya 2011, inazuia yeyote anayewania kiti cha kisiasa kushiriki katika harambee miezi minane kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Hata hivyo, Dkt Ruto aliendelea kushirikiana na viongozi wa makanisa huku wakimtembelea katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

Mnamo Alhamisi, viongozi wa makanisa chini ya Shirikisho la Makanisa ya Kiinjilisti na Kiasili ya Kenya, waliunga azima ya urais ya Dkt Ruto anayewania kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Hii ilikuwa siku moja baada ya viongozi hao kumtembelea katika makazi yake Karen ambapo alikubali kwa kutia saini kutekeleza matakwa yao iwapo atashinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Siasa ni maslahi na viongozi wa makanisa wana maslahi yao. Ninafurahi wameamua kuwa upande ambao maslahi yao yatazingatiwa,” Dkt Ruto alisema alipohutubia viongozi wa kidini waliokusanyika Karen mnamo Alhamisi asubuhi.

Kulingana na mwenyekiti wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjilisti na Kiasili ya Kenya, Askofu Samuel Njiriri, waliamua kumuunga Dkt Ruto kwa sababu ya imani yake kama Mkristo.

Askofu huyo alisema walichunguza viongozi wote wanaowania uongozi wa nchi, na wanaridhika kwamba Dkt Ruto ndiye anayetosha kumrithi Rais Kenyatta.

“Kama viongozi wa makanisa chini ya shirikisho letu, tayari tumetangaza msimamo wetu, tutaunga kiongozi anayemcha Mungu na anayejali maslahi ya watu wetu,” alisema.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba hatua ya viongozi wa makanisa kumuunga Dkt Ruto inatokana na ukarimu wake kwao ambao umewafanya mateka wakitarajia kwamba atawafaa zaidi iwapo atashinda urais na kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Dkt Ruto amekuwa akisaidia viongozi wa kidini na makanisa yao kwa michango tofauti licha ya kukosolewa na wapinzani wake wanaotilia shaka chanzo cha pesa anazochanga. Ukarimu wake umewafanya viongozi wengi wa kidini mateka wakitarajia makuu zaidi kutoka kwake iwapo ataibuka mshindi wa urais na kuunda serikali,” asema mchaganuzi wa siasa Geff Kamwanah.

Hata hivyo, alisema viongozi wa kanisa Katoliki na Kiangilikana, kwa kawaida huwa hawachukui msimamo wa wazi wakati wa uchaguzi mkuu.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakiwalaumu viongozi wa makanisa kwa kutekwa nyara na michango ya Dkt Ruto bila kujali chanzo cha mamilioni ambayo alikuwa akitoa kwenye harambee kabla ya Februari 2022.

Ingawa hawajawahi kuthibitisha, wapinzani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimlaumu kwa kuonyesha ukarimu akitumia pesa za ufisadi.

Licha ya shutuma kali kutoka kwa Rais Kenyatta, viongozi wa kidini, wakiwemo maakofu 17 wanachama cha Shirikisho la Makanisa la Kievanjelisti na Kiasili ya Kenya wamegandwa kwa Dkt Ruto wakisisitiza kuwa ni kiongozi mcha Mungu na anajali watu masikini.

  • Tags

You can share this post!

Spurs walazimishia Liverpool sare katika EPL ugani Anfield

Tim Wanyonyi sasa ndiye mwaniaji ubunge Westlands kwa...

T L