• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Umaarufu wa Kidero tishio kwa ubabe wa ODM Nyanza

Umaarufu wa Kidero tishio kwa ubabe wa ODM Nyanza

NA GEORGE ODIWUOR

WACHAMBUZI wa masuala ya siasa wanasema kuwa uchaguzi wa Agosti utakuwa mtihani mgumu kwa kinara wa ODM, Raila Odinga kwa kuwa wapigakura katika maeneo yanayoaminiwa kuwa ngome yake huenda wakakosa kuzingatia maagizo yake ya kuwachagua wawaniaji wa mrengo mmoja (suti).

Ikiwa chama hicho maarufu katika Kaunti ya Homa Bay kitapoteza kiti cha ugavana na viti vya ubunge, wachambuzi wanasema huo utaashiria mwanzo wa mwisho wa utawala wa kisiasa wa Bw Odinga katika kaunti hiyo.

Ushawishi wa Bw Odinga ulikifanya chama hicho kushinda viti 38 kati ya 40 vya wadi, viti vyote vinane vya ubunge, seneti, mwakilishi wa kike na kiti cha ugavana katika kaunti hiyo katika uchaguzi uliopita.

Baadhi ya wanaowania nyadhifa mbalimbali kupitia ODM wamepingwa vikali kwa kujaribu kuendeleza mfumo huo wa suti.

Mnamo Julai 3, Bw Odinga alizuru kaunti hiyo na kujipigia debe katika maeneo mbalimbali kama vile Kasipul, Suba, Ndhiwa na Homa Bay na kuwaomba wakazi wa maeneo hayo kuwapigia kura wanasiasa wanaowania kwa tikiti ya ODM pekee.

Wakati wa kampeni, Bw Odinga aliendeleza mfumo huo wa suti huku akiwasimamisha wawaniaji wote wa nyadhifa mbalimbali kwa tikiti ya ODM.

Hata hivyo, ziara yake katika kaunti hiyo haikuzaa matunda kwani wakazi wa kaunti hiyo hawajakumbatia mfumo huo wa kupiga kura.

Kiti cha ugavana katika kaunti hiyo kimezua mzozo kati ya mwakilishi wa kike, Gladys Wanga wa ODM na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero ambaye ni mwniaji huru.

Mark Raudi wa UDA ndiye mwaniaji wa tatu wa kiti hicho ila umaarufu wake hauwezi kulinganishwa na wa Bi Wanga na Dkt Kidero.

Japo kura ya maoni haijatolewa kuhusu watatu hao, ni vigumu sana kufahamu ni nani kati yao atakayeibuka mshindi.

Hata hivyo, kulingana na wachambuzi wa siasa, Bi Wanga na Dkt Kidero wana nguvu sawa na huenda yeyote kati yao akaibuka mshindi.

Walter Opiyo, kiongozi wa ‘Bunge la Wananchi’ katika kaunti hiyo, kundi ambalo linachambua masuala ya siasa katika eneo hilo, alisema kuwa atakayeibuka mshindi kati ya wawili hao atamshinda mwenzake kwa kura zisizozidi mia moja.

“Kuna ushindani mkubwa kati ya wawili hao. Huenda uchaguzi ukafanywa tena katika kaunti hii. Hivi sasa wapigakura wote wameshafanya uamuzi kuhusu watakayemchagua,” akasema Bw Opiyo.

Kadhalika, Bw Opiyo alisema ushindi wa Bi Wanga utamletea afueni kiongozi huyo wa chama cha ODM kwani matakwa yake yatakuwa yametimizwa.

Hata hivyo, ushindi wa Dkt Kidero utatatiza umaarufu wake katika kaunti hiyo kwani utafungua ‘macho’ ya wapigakura kwamba lazima wasielezwe ni nani wa kumchagua, badala yake wampime kila mgombeaji na kumchagua wanayemdhania kuwa bora.

“Kaunti haijawahi kuongozwa na mgombeaji huru. Lakini ushindi wa mgombeaji wa ugavana huru utafungua milango kwa wagombeaji wengine huru katika chaguzi zijazo.”

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Hadaa za viwanja, kulikoni?

Raila ‘aoshwa laana ya 1969’

T L