• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Unga: Chapa zinazopendwa zingali ghali

Unga: Chapa zinazopendwa zingali ghali

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI sasa inasema bei ya unga wa mahindi imeanza kushuka, ishara kuwa gharama ya maisha inayowaathiri Wakenya wengi imeanza kushuka.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed alisema Jumatatu Aprili 17, 2023 kwamba bei ya paketi moja ya kilo mbili imeshuka hadi Sh159 na Sh160, kulingana na kampuni ya usagaji iliyopakia unga wenyewe.

Bw Mohamed alisema kushuka huko kwa bei kunafuatia ahadi aliyotoa Rais William Ruto wiki jana kwamba bei ya bidhaa hiyo itaanza kushuka kuanzia wiki hii.

“Bei ya unga imeanza kushuka jinsi Rais William Ruto aliwahakikishia Wakenya wikiendi iliyopita. Bei zimeshuka hadi Sh159 na Sh160 ikilinganishwa na kampuni ambako unga huo ulisagwa. Rais Ruto alipoingia afisini mnamo Septemba 13, 2022, paketi ya kilo mbili ya unga wa mahindi ulikuwa ukiuzwa kwa bei ya reja reja ya Sh230,” Bw Mohamed akasema kwa njia ya Twitter.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika maduka kadha jijini Nairobi ulibaini kuwa unga wa mahindi chapa UMI ndio uliokuwa ukiuzwa kwa Sh159 kwa paketi moja ya kilo mbili.

Chapa maarufu na zinazopendwa na wateja wengi kama vile Pembe, Soko na Jogoo bado zilikuwa zikiuzwa kwa kati ya Sh208 na Sh220. Nao unga wa mahindi chapa Raha ulikuwa ukiuzwa kwa bei ya Sh252 kwa paketi moja ya kilo mbili katika matawi kadhaa ya supamaketi ya Naivas, katikati mwa jiji la Nairobi.

Akiongea Ijumaa katika eneo la Mavoko, Kaunti ya Machakos, Rais Ruto alikariri kuwa serikali imejitolea kupunguza gharama ya maisha.

“Tumeanza kwa kusambaza mbolea ya bei nafuu kwa wakulima wetu ili waweze kuzalisha chakula kingi kuanzia Agosti mwaka huu. Kabla ya wakati huo, tumeagiza mahindi kutoka nje na yatawasili kesho (Jumamosi). Hivyo kuanzia wiki ijayo bei ya unga itaanza kushuka,” Dkt Ruto akasema.

Alisema hayo alipokuwa akiwahutubia wananchi baada ya kuzindua mradi wa maji uliogharimu Sh2.7 bilioni.

Hata hivyo, viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wanashikilia kuwa wanataka bei ya unga kushuka hadi Sh100 kwa paketi moja ya kilo mbili, alivyoahidi Rais Ruto wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Lakini alipoingia mamlakani mnamo Septemba 13, 2022 Rais Ruto alifutilia mbali mpango wa serikali wa ruzuku kwa bei ya unga, mpango ulioanzisha siku za mwisho za utawala wa mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta.

Chini ya mpango huo, unga ulipaswa kuuzwa kwa Sh100, lakini bidhaa hiyo iligeuka kuwa adimu kiasi kuwa ni maduka machache yaliyouza unga huo.

Akifutilia mbali mpango huo, Rais Ruto alisema kuwa mpango huo haukuwa na manufaa kwa wananchi licha ya kwamba uligharim Sh7 bilioni, pesa za mlipa ushuru.

“Mlipa ushuru aligharimia mpango huo kwa Sh7 bilioni ili unga uuzwe kwa Sh100. Lakini unga huo haukupatikana kwa urahisi. Ikiwa hizo Sh7 bilioni zingetumika kununua mbolea na kuwasambazia wakulima, hali ingekuwa tofauti,” akasema Rais Ruto.

“Hii ndio maana tumeamua kupunguza gharama ya uzalishaji chakula kwa kuanzisha mpango wa usambazaji mbolea wa bei nafuu ya Sh3,500 kwa gunia moja la kilo 50. Tumefutilia mbali mpango wa ruzuku kwa sababu ulikuwa unawafaidi matajiri wachache huku Wakenya wakiumia,” akaeleza kwenye mkutano wa kundi la wabunge wa Kenya Kwanza mjini Naivasha, Septemba 28.

Lakini katika siku za hivi karibuni, Azimio imekuwa ikiishinikiza serikali kurejesha mpango wa ruzuku kwa bei ya unga ili bidhaa hiyo iuzwe kwa Sh100 kwa paketi ya kilo mbili.

  • Tags

You can share this post!

Mitishamba imejaa sumu, utafiti wabaini

Kampuni ya maji yajengea shule darasa la kisasa

T L