• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
UPWEKE: Mji wa mtu mmoja pekee

UPWEKE: Mji wa mtu mmoja pekee

MASHIRIKA na PETER MBURU

JAPO mapenzi ya watu ni kuishi karibu na watu wengine na kutenga muda mwingi kuzungumza na watu, mama mmoja wa miaka 84 kutoka Marekani amekuwa akiishi katika mji peke yake.

Hii ni kutokana na hali kuwa watu waliokuwa katika mji huo aidha wamefariki ama kuhama, hivyo akiachwa peke yake, lakini Bi Elsie Eiler, 84, anasema kuwa furaha yake ni kuishi eneo hilo na kuwa hawezi kuhama hata kuwe nini.

Unapowasili katika mji wa Monowi, jimbo la Nebraska, Amerika kinachokukaribisha ni hewa safi na utulivu, japo uwepo wa watu kama ilivyo kawaida ya mji wowote ule hapa haupo.

“Ni mimi peke yangu ninayeishi hapa mjini, watu wengine wote aidha wamekufa ama kuhama, lakini hapa ndipo niliamua kuishi,” anasema Bi Eiler.

Anasema kuwa wazazi wake walihamia takriban nusu ya maili kutoka mji huo miaka 14 iliyopita na tangu wakati huo amekuwa akiishi huko peke yake.

Japo ana watoto wawili, walichoshwa na upweke wa kuishi mji usio na watu na kuhama, lakini ajuza huyo anasema huko ndiko nyumbani na kamwe hawezi kuhama.

“Nina mvulana na binti lakini wote wameenda kuishi mbali baada ya kukamilisha masomo. Watu huuliza ikiwa hawanijali ninawaambia wananijali lakini pia wanaheshimu kauli yangu kuwa hivi ndivyo nimependa kufanya,” ajuza huyo asema.

Bi Eiler hujijukumisha ili kuhakikisha kuwa shughuli za mji wake mdogo zinaendelea kama kawaida kwa kuwa kila siku anapokea wageni kutoka majimbo na mataifa mbalimbali wakifika kujionea upekee wa mji huo na mmiliki wake.

“Huwa ninafungua baa saa tatu asubuhi na kuna malori na wauzaji wanaofika kuleta vinywaji na wateja pia, huku wengine wakija tu kujiburudisha kwa kahawa,” akasema.

Anasema wengine huacha jumbe kwa wenzao watakaofika ama vitu vingine, hizo zikiwa ni baadhi ya shughuli za kuendesha uchumi wa mji huo.

“Huwa wanapiga kusikia ikiwa wenzao wako hapa. Ni sehemu ya watu kukutana hivi na nadhani kila mtu hujihisi amekaribishwa kufika hapa. Kila mtu anahitaji eneo kama hili nadhani, nikiwa mmoja wao.”

Lakini je, usimamizi wa mji huu huwa vipi?

Kwa kuwa mkazi ni mmoja, Bi Eiler anasema kwa hali hiyo anaishia kuwa usimamizi mzima wa mji huo akiwa peke yake hivyo, akijiita kuwa meya na bodi ya usimamizi wa mji kwa pamoja.

“Kwa kuwa ni mimi tu niko hapa mjini, kuna majukumu mengine kando na baa, mimi ndiye meya na bodi ya usimamizi wa mji kimsingi,” asema Bi Eiler.

“Lakini pia sihitaji kujali kuhusu uchaguzi kwa kuwa hakuna ushindani wa aina yoyote. Wakati mwingine ninasutwa kutokana na hilo lakini ninawaambia watulie kwa kuwa hawako katika sehemu ya mji wangu na hivyo hawawezi kupiga kura huku.”

Bibi huyo alisema kuwa watu kutoka majimbo 47 ya Marekani na mataifa 42 ya ulimwengu wamezuru mji huo, ambao maelezo yake ni kuwa watu huuona “kuwa wa maajabu na kushangaza.”

Hata hivyo, licha ya kuwa baadhi ya watu wamejaribu mbeleni kumsihi aishi karibu na watu, Bi Eiler anasema kuwa “Kwa kweli sina matamanio yoyote ya kuishi mahali popote, nimeridhika kabisa nilipo sasa.”

You can share this post!

Romania yataja kikosi kitakachovaana na Simbas Bucharest

#GoogleWalkOut: Wafanyakazi wagoma kulalamikia dhuluma za...

adminleo