• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
URAIBU WA POMBE: ‘Githeri Man’ angali mtumwa wa chang’aa

URAIBU WA POMBE: ‘Githeri Man’ angali mtumwa wa chang’aa

Na SAMMY WAWERU

MARTIN Kamotho Njenga aliibua ucheshi mitandaoni na katika vyombo vya habari wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, picha zake akiwa kwenye foleni ya kupiga kura akipakata karatasi ya na plastiki iliyotiwa githeri ziliposambaa.

Tukio hilo lilimvunia umaarufu nchini, na kuishia kupata jina la lakabu ‘Githeri Man’.

Baadhi ya mashirika yalijitokeza kumpiga jeki kifedha, kwa kile kilichotajwa kama jitihada kuonesha uzalendo kushiriki zoezi la kidemokrasia kuchagua viongozi anaotaka akistahimili jua kali, machovu ya kusimama katika laini ya kura kwa njia ya kipekee.

Ni suala ambalo lilimfanya kuwa miongoni mwa waliozawadiwa na Rais Uhuru Kenyatta katika tuzo ya kiongozi wa taifa, Head of State Commendation, mwaka huo wa uchaguzi.

Hata hivyo, mwaka uliofuata, 2018, Bw Kamotho alimrai Rais Kenyatta kumnusuru kutoka kwa minyororo ya unywaji wa pombe.

Martin Kamotho Njenga akionyesha cheti cha kufuzu mafunzo ya kubadilisha tabia na maadili kutoka kituo cha Mamacare. Picha/ Sammy Waweru

Ombi la kutaka kuiasi lilimfikia Rais kupitia dereva wake, Kenyatta alipohudhuria hafla ya kutoa hatimiliki za mashamba bustani ya Jacaranda jijini Nairobi.

Aidha, Rais aliamuru mwakilishi wa wanawake Kiambu Gathoni Wa Muchomba kumsajili katika kituo cha kurekebisha tabia na maadili cha Mamacare kilichoko Wangunyu na anachokiongoza kama patroni, ili kumnasua dhidi ya kero la pombe.

“Niliambia dereva wa Rais amfikishie ujumbe ninaomba anisaidie kuenda rehab (kituo cha kurekebisha waathiriwa wa pombe na dawa za kulevya kupindukia. Nilijiunga na Mamacare mwezi Mei,” akasema Kamotho.

Githeri Man pamoja na waraibu wenza wa pombe na dawa za kulevya walifuzu na kupokea cheti cha maadili mema katika hafla iliyohudhuriwa na Rais Desemba 2018.

‘Githeri Man’ wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali kwa nyumba yake hapo Februari 5, 2019. Picha/ Sammy Waweru

Licha ya mafunzo hayo, amerejelea tena unywaji wa mvinyo, hasa ile haramu na anamuomba kiongozi wa taifa ‘kumuokoa’. Anasema Bw Kenyatta alikuwa amempa ahadi ambayo hakuifichua, ikiwa atahitimu mafunzo.

Ahadi ya Rais ilipania kumsaidia kuacha unywaji wa pombe ambao umeonekana kulemaza ndoto zake. “Ninamshukuru kwa dhati kwa kujitolea kunisaidia niache kuwa mateka wa pombe. Aliniahidi nikimaliza kurekebikisha tabia atanizungumzia, ningali ninasubiri,” akasema.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, Bw Kamotho ameeleza kwamba baada ya kuhitimu, alipaswa kupata mafunzo ya kozi ya kiufundi kama vile useremala na uashi, katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Kilimambogo, Thika.

“Nilienda Kilimambogo kwa siku tatu pekee, nikatoka. Lengo langu lilikuwa mafunzo ya kuacha pombe, sihitaji kozi nyingine kwa sasa kwa sababu nimesomea umekanika,” akafichua.

‘Githeri Man’ (wa tatu kushoto) akiwa na waraibu wenzake wa pombe na dawa za kulevya katika kituo cha kurekebisha tabia cha Mamacare, Kiambu, Julai 24, 2018. Picha/ Sammy Waweru

Chang’aa ya Sh5

Ni mzaliwa wa Githunguri, Kiambu ingawa anafanya kazi Nairobi. Kiambu ni mojawapo ya kaunti zilizoathirika pakubwa kwa unywaji wa pombe. Gavana Ferdinand Waititu na Bi Wa Muchomba wamekuwa wakiendesha kampeni ya kudhibiti kero hili.

Githeri Man, mkwasi wa ukarimu, alizaliwa mwaka wa 1975 na ni mzaliwa wa pili katika familia ya watoto watano. Anasema alisitisha masomo yake ya shule ya msingi katika darasa la saba mnamo 1989. “Ulikuwa uamuzi wa kibinafsi, nikajitosa katika sekta ya matatu kama utingo ambapo pia nilisomea umekanika,” asimulia.

Anadokeza kwamba alianza unywaji wa pombe, haswa chang’aa akiwa na umri wa miaka 17 katika mtaa wa mabanda wa Mathare, jijini Nairobi.

Akivuta mawazo nyuma, anakumbuka kana kwamba ilikuwa jana tu mwaka 1992 alifukuzwa na mama yake baada ya kufanya kosa na ndipo safari ya kuwa mteja wa chang’aa iling’oa nanga.

Akisukuma toroli aliyopaswa kuitumia kupata mafunzo ya kiufundi katika taasisi ya Kilimambogo, Thika. Picha/ Sammy Waweru

“Alitufukuza pamoja na mjomba. Tulikuwa na Sh15 pekee, tukafululiza hadi mtaa wa Mathare ambapo alinijuza kunywa chang’aa,” aeleza akifichua kuwa walibugia pombe yenye thamani ya Sh5, na ambayo imekuwa kibarua kuiacha kufikia sasa. Glasi moja ya chang’aa wakati huo iliuzwa Sh2.50.

Kwa kuwa wasingerudi nyumbani kwa hofu ya kuadhibiwa na mama, anasema siku hiyo aliingia barabarani ikizingatiwa alikuwa makanga na pesa alizopata alikodi chumba lojing’i ambako walijisitiri kwa muda.

“Nilikuwa nikilipa Sh50 kwa siku, lojing’i ikawa makazi yetu kwa muda. Jioni baada ya kazi tusingekosa kupitia Mathare kufungua mwasho wa koo,” anasema Githeri Man kwa ucheshi. Baadaye mjomba alimuachia usukani wa kunywa pombe, akaokoka 2010 na hata kupata jiko.

Madaraka

Mwaka 1999 Githeri Man aliajiriwa katika halmashauri ya jiji la Nairobi kama mfagiaji wa mabustani, barabara na kusafisha mitaro ya majitaka, anakohudumu kufikia sasa ingawa baada ya kupata tuzo ya Head of State Commendation 2017 alipandishwa madaraka.

Kabla ya kuwa tajika, anasema nyakati nyingi aliponea tundu la sindano kupigwa kalamu kwa sababu ya kutekwa na pombe.

Akisukuma rukwama katika shughuli za usafi. Picha/ Sammy Waweru

Wakati wa mahojiano, mjombake Moses Mwangi alisema unywaji wa Kamotho si wa kawaida, na kwamba una chanzo chake kwa sababu amejaribu kadri awezavyo kumshauri aache, juhudi zake zikigonga mwamba. Alisema mzongo wa mawazo huenda ukawa mojawapo ya kiini kikuu.

“Unywaji wa pombe hauji kwa ajili ya uraibu pekee. Martin Kamotho ana mzigo unaomfanya kuwaza sana na unahitaji kuatuliwa kwani huenda ndio sababu kuu ya kunywa kupita kiasi,” akasema Bw Mwangi.

Kimsingi shinikizo la marafiki na taabu ni vigezo vinavyonyooshewa kidole cha lawama kwa wanaokunywa pombe kupindukia, kulingana na Kasisi Charles Kinyua ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia.

“Mzongo wa mawazo utokanao na shida za kimaisha hupelekea mwathiriwa kujihusisha na visa vya unywaji wa pombe na utumizi wa dawa za kulevya,” asema Bw Kinyua.

Anahimiza haja ya familia ya mwathiriwa kujua kiini cha mhusika kuzongwa na mawazo, ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wa kisaikolojia.

You can share this post!

CATHERINE NYOKABI: Ndoa ya harusi ilivyoishia kwa talaka

Amuua mumewe kwa sumu ili aolewe na mpenzi wake mfungwa

adminleo