• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Utangamano wa kitaifa ni moja ya malengo muhimu ya elimu, tuuthamini!

Utangamano wa kitaifa ni moja ya malengo muhimu ya elimu, tuuthamini!

Na ALI SHISIA

Jitihada zinazofanywa na wanajamii wa kila nui kuhakikisha wanao wanapata elimu hukusudia jambo moja; wana hao wanaowahangaikia waimarike.

Kuimarika huku hutofautiana toka mtu mmoja hadi mwingine. Wapo wanaotamani wanao wajifunze kujieleza.Wapo wanaotegemea wanao wazitambue au kuzikuza talanta zao ama yote mawili. Asilimia kubwa zaidi hutaraji wanao wapate ajira baada ya kufuzu masomoni ili wakidhi mahitaji yao wenyewe na ya wazee wao ikiwezekana.

Hivi serikali ambayo imekuwa ikigharamia asilimia fulani ya karo ya wanafunzi hawa hukusudia nini? Hutegemea nini hadi ikagharamia kiasi kikubwa cha elimu ya shule za msingi na za sekondari (kwa wanafunzi wa kutwa)? Kuandaa wataalamu wa sekta mbalimbali katika soko la ajira la nchi hii ni mojawapo ya azma za serikali. Maendeleo ya kitaifa ni lengo jingine muhimu lakini orodha hii haikamiliki kabla ya kutaja umoja na utangamano wa kitaifa.

Maswala yote tuliyoyataja awali ni muhimu lakini yana umuhimu wenye mawanda finyu; yaani ni faida ya mtu binafsi au familia. Umoja wa kitaifa ni lengo linalonuia kuvuka mipaka ya kidini na kikabila, kitabaka na kiitikadi ili kujinufaisha kadri iwezekanavyo toka kwa mwananchi mwenzio.

Hivi ni kwa msingi kwamba mengi ya mambo haya tuyaonayo kama vyanzo vya kututambulisha na kututenganisha ni matukio ya kisadfa. Ama yupo miongoni mwetu anayeweza kudai kwamba alinuia kuzaliwa katika kabila fulani na ikawa hivyo? Je kunaye anayeweza kudai kwamba katu hawezi kuoa au kuolewa na mtu wa kabila fulani? Wengi wamewahi kujitungia sheria za jinsi hii na mioyo yao ikawalazimu kuzivunja walipokutana na wahibu wao walioandikiwa na Mwenyezi Mungu.

Ikiwa elimu yetu, kisomo chetu hakituelekezi katika kuthaminiana pasi na kujali usuli wetu kidini na kikabila basi afadhali tuikome na kujishughulisha na mambo tofauti.Katika kipindi hiki ambapo joto la kisiasa linazidi kupanda nchini, wanafunzi twapaswa kuwa katika mstari wa mbele kukariri haki na amani bila kujali misingi ya kikabila.

Ama mbona wazazi wajitahidi wanao wajiunge na shule za sekondari za kitaifa huku imani na misimamo yao ikisalia kuwa ya kijijini? Ni utaifa upi tunaoutafuta tunapowataka wana wetu wasomee shule za hadhi za kitaifa lakini tukazidi kuwasisitizia jinsi wenyeji wa baadhi ya makabila yaliyowakilishwa shuleni mwao yasivyofaa?Wakati umewadia kwetu sote, wakubwa kwa wadogo, wazazi na wana wetu kuwaona wenzetu kama vijalizo vya dhaifu zetu.

Yaani, uzione thurati za kabila lako kama zisizokamilika hadi zinapounganishwa na za makabila mengine. Ukitazama kwa makini utagundua Mwenyezi Mungu amegawa raslimali zake kwa njia isiyosailika. Amekupa huu akakunyima huu; chambilecho Waswahili: una huu na huu hauna.

Kwa jinsi hii kila mmoja wetu ahitaji uzoefu na tajriba ya mwenziwe aliyekulia mazingira tofauti ili akamilike kimawazo na kuibuka na mbinu mpya za utatuzi wa migogoro.Yeyote miongoni mwetu kujihisi kakamilika bila mchango na msaada wa mwenziwe ni kujitia kiburi kinachoweza kumporomosha na mapema.

Tujifunze kuwathamini ndugu zetu wa makabila mengine na dini tofauti na zetu. Huku ndiko kukomaa kunakohitajika hasa katika kipindi hiki. Vijana, wanafunzi tuna nafasi muhimu pamoja na idadi yetu kubwa kuzuia ghasia nchini.

Unapotofautiana na mwenzio kimawazo, kimtazamo au kimsimamo, usiwe mwepesi kuamua kwamba ni kwa sababu yuatoka katika kabila tofauti na lako bali kwa sababu ya uelewa wenu tofauti wa jambo lile lile, au hujawahi kutofautiana na mzaliwa nawe mnayefaana licha ya kufanana kama shilingi kwa ya pili? Yatafakari haya kabla ya kuchukua hatua kumvamia mwenzio au kuharibu mali yake aliyoyapata kwa kumwaga jasho jingi.

You can share this post!

Vissel Kobe inayoajiri Mkenya Masika iko mguu mmoja nje ya...

Raila atetea miradi ya handisheki