• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:25 PM
Uthiru Vision tumepania kushriki ligi kuu Kenya lakini ufadhili balaa

Uthiru Vision tumepania kushriki ligi kuu Kenya lakini ufadhili balaa

Na JOHN KIMWERE
TAIFA hili limefurika timu nyingi tu za wachezaji chipukizi wanaume na wanawake ambazo huwa zimejifunga nira kupalilia talanta za wahusika huku wakilenga kutinga hadhi ya juu miaka ijayo.
Mchezaji yoyote huanza kunoa makucha ya fani yake huku akilenga kukomaa kutinga kiwango cha kimataifa. Wanasoka wa Uthiru Vision FC ni miongoni mwa vikosi 14 ambavyo vimepangwa Kundi A kwenye mechi za kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu.
”Tayari tumejikuta kwenye wakati mgumu kwa kukosa ufadhili ingawa tumepania kujikaza mithili ya mchwa tukilenga kumaliza kati ya tano bora katika msimamo wa mechi za msimu huu,” kocha wake, Philip Odhiambo alisema na kuongeza kuwa kampeni za msimu huu hazikuwa mteremko.
Anadokeza kuwa kila muhula ligi zote huonyesha kibarua cha kufa mtu. Katika mpango mzima kocha huyo anasema kuwa ingawa wanawazia kufuzu kushiriki Ligi Kuu miaka ijayo watakuwa pazuri na tayari watakapopata mfadhili.
Uthiru inashiriki ngarambe hiyo kwa mara ya pili baada ya kumaliza kati ya kumi bora msimu uliyopita. Kati ya mechi sita ambazo wamebakisha kocha huyo anasema patashika yao na Makarios 111 (Riruta United) kamwe haitakuwa rahisi.
”Wachana nyavu wa pande zote wanafahamu patashika hiyo haitakuwa mteremko kwa kuzingatia watakuwa kazini kusaka pointi tatu muhimu kuwaongezea tumaini la kufanya kweli,” akasema. Katika jedwali la kipute hicho, Uthiru Vision FC imetua nafasi ya sita kwa kuzoa pointi 30 baada ya kushiriki migarazano 20.
Pandashuka
Anasema ukosefu wa ufadhili umeibuka donda sugu kwa timu nyingi ambapo huwa vigumu kwa klabu yoyote kuweka misingi ya kufuzu kushiriki ligi za juu. ”Uhaba wa ufadhili huchangia timu nyingi kushindwa kuweka mikakati mwafaka kufanikisha maazimio yazo michezoni,” akasema.
Uthiru Vision inayojivunia kulea David Beckham aliyejiunga na Tandaza FC iliasisiwa mwaka 2007 na marehemu Cosmus Muchiri ili kunoa kucha za wachezaji chipukizi katika eneo la Dagoretti Kusini.
Kikosi hicho hufanyia mazoezi katika Uwanja wa Ahiti, Dagoretti Kusini. Klabu hii inajivunia huduma za wachezaji bora ikiwamo Kelvin Kinyanjui (nahodha), Samuel Kuria, Stephen King’ori, Stephen Masakari na Dancun Kimathi.
Pia inajumuisha Arnold Otechi, Christopher Oponyo, Ferdinand Malimba, Geoffrey Kamau, Billy Robert, Peter Chege, Patrick Chege, Arnold Majani, Caleb Ombuna na Joseph Mbugua.
  • Tags

You can share this post!

Wahitimu 6,500 kutoka MKU washauriwa wawe wabunifu

DOUGLAS MUTUA: Wakenya watumie akili kabla ya mambo...