• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Uwanja ambapo ibada hufanyika wakati wa corona

Uwanja ambapo ibada hufanyika wakati wa corona

Na SAMMY WAWERU

Ni zaidi ya siku 100 tangu kisa cha kwanza cha maambukizi ya Covid – 19 kiripotiwe nchini Kenya, mnamo Machi 13, 2020.

Kudhibiti maambukizi, sheria na mikakati maalum ilitolewa chini ya maelekezi ya Wizara ya Afya kwa mujibu wa vigezo vya Shirika la Afya Duniani, WHO.

Inajumuisha uvaliaji barakoa ndiyo maski katika maeneo ya umma, kuzingatia umbali wa zaidi ya mita moja na nusu kati ya mtu na mwenzake, unawaji mikono kila wakati, na pia kuepuka maeneo ya umma.

Mikusanyiko au makongamano katika maeneo ya kuabudu, mabaa na vilabu, na mikutano ya hadhara kijumla, ilipigwa marufuku kwa muda, ili kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya corona, ambavyo kwa sasa ni kero la ulimwengu mzima.

Kimsingi, ni mikakati ambayo imetajwa kuchangia kudorora kwa uchumi, japo serikali inashikilia haina budi ila kuhakikisha inatekelezwa kwa kile inahoji “maisha ya Wakenya ni muhimu zaidi kuliko uchumi”.

Licha ya maeneo ya kuabudu kupigwa marufuku Machi 2020 kwa muda usiojulikana, imebainika baadhi ya watu wanakongamana kisiri ili kulishwa chakula cha kiroho na wachungaji wao.

Mtaa wa Membley, ulioko katika eneo la Ruiru, kaunti ya Kiambu, na karibu na Thika Super Highway ni wa kifahari na unaoishi mabwanyenye, kwa mujibu wa taswira ya nyumba zilizojengwa humo, sawa na kasri la mfalme.

Katika mtaa huo, pembezoni ni uga mkubwa ulioshikana na Thika Road, kati ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (K.U) na Bypass – Ruiru.

Kufika katika uwanja huo, unaingilia eneo maarufu la Clayworks. Ni katika uwanja huohuo ambapo kila Jumapili makundi mbalimbali ya watu hukongamana kusifu, kuabudu Mungu na kupokea chakula cha kiroho.

Katika uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali wa muda wa wiki tatu mfululizo, imefichuka shughuli hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu.

Mojawapo ya Jumapili, tunaungana na kundi moja la washirika, tukiarifiwa kwamba kila kundi linawakilisha kanisa.

Mwendo wa saa tano hivi za asubuhi, tunatua eneo la Clayworks, na katika uga huo tunakaribishwa na sauti za ngoma, nyimbo za kuabudu na maombi ya toba, matukio yanayohinikiza anga tua hiyo. “Huwa tunakongamana humu kila Jumapili na Alhamisi kukata kiu cha chakula cha kiroho,” mmoja wa muumini anadokeza.

Uwanja huo umegawanywa mara mbili na barabara inayoelekea mtaa wa kifahari wa Membley. Pia, reli ya zamani inayounganisha jiji la Nairobi na Nanyuki na ambayo inafufuliwa imepitia humo.

Kwa kupepesa macho, kila uga una makundi tofauti ya washirika, ambao wamekusanyika kwa kuunda umbo la mviringo.

Kabla ya ibada kuanza katika kundi lililotualika, washirika na makuhani wanaingia katika maombi yanayochukua muda wa takriban dakika thelathini. “Kila siku huwa tunatangaziwa maambukizi mapya ya virusi vya corona na pia wagonjwa waliofariki. Ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu sisi kuwa hai, na huwa tunakusanyika hapa kumshukuru,” pasta anayejitambua kwa jina Muia anaiambia Taifa Leo Dijitali.

Baada ya kusali, pasta mkuu anaanzisha ibada. Inashirikisha ulishaji wa chakula cha kiroho kwa waumini na pia nyimbo za kumtukuza Mungu.

“Mambo ni magumu, ila tunaelekeza macho yetu kwa Mwenyezi Mungu atuondolee janga la corona. Licha ya ugonjwa huu kuwa kikwazo, hatutakoma kumshukuru,” mhubiri anaeleza katika mahubiri.

Aidha, anashirikisha waumini kadhaa kutoa ushuhuda na pia kuhubiri.

Gladys Wambura, anasimulia masaibu aliyopitia baada ya kupoteza wapendwa wawili na anaungama Mungu aliwawezesha kuwapumzisha licha ya changamoto zilizopo.

“Sote tukifuata na kuiga maandiko katika kitabu cha pili cha Timothy 2 : 20 – 21 tutaishi kufurahia neema za Mungu,” kijana Samuel Muigai anahimiza katika mahubiri.

Kipindi cha kutukuza kwa njia ya nyimbo, ndicho kinaibua maswali. Kigezo cha umbali kati ya mtu na mwenzake, kinakiukwa, ikizingatiwa kuwa ni vigumu kuzuia watu kutangamana wakati wa kuimba.

Washirika wote wanatumbuiza bila kukumbuka hatari inayowakodolea macho, kuambukizwa virusi vya corona endapo kuna mgonjwa miongoni mwao. “Hii ni fursa ya kipekee ambayo huwa haipatikani kwa urahisi, hivyo basi tujiwachilie kwa kusifu,” pasta mkuu anaeleza.

Ibada ya misa inaendelea, na pia matoleo ya sadaka yanafanyika, katika kundi hilo la kanisa ambalo lilikuwa na washirika wapatao 43. 

Ni taswira inayoshuhudiwa katika makundi mengine, na kulingana na hesabu yalikuwa zaidi ya 20.

Kundi moja la dhehebu la Akorino, kamwe washirika hawazingatii umbali kati ya mtu na mwenzake. Wanatangamana bila wasiwasi, watoto wakiwemo.

Isitoshe, hakuna aliyevalia barakoa, na kadhaa kifaa hiki muhimu kuzuia kuambukizwa Covid – 19 kinaning’inia kwenye kidevu.

Katika uwanja huo ambao pia hutumika katika soka na michezo mingineyo, kuna wanaoshiriki maombi wakiwa binafsi.

Ni mikusanyiko ambayo inatekelezwa licha ya serikali kupiga marufuku makongamano ya aina yoyote yale.

Mnamo Jumapili Juni 21, 2020, siku 100 baada ya Kenya kuthibitisha kuwepo kwa virusi vya corona nchini, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisisitiza kwamba mikusanyiko ya watu ingali marufuku. “Hakuna mikusanyiko ya aina yoyote ile inayokubalika katika Jamhuri ya Kenya kipindi hiki, kwa sababu inahatarisha maisha ya watu wetu,” Waziri Kagwe akasema.

You can share this post!

Uuzaji wa sidiria umempa riziki kwa miaka mitano

‘Kusuka mabinti na kuwarembesha kucha ni riziki...

adminleo